Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma (pichani) amesema sensa ya watu na anuani za makazi inayoratibiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaisaidia Mahakama ya Tanzania kupanga upya mpango wa ujenzi wa miundombinu, ikiwemo ujenzi wa Mahakama mbalimbali hapa nchini.
Mhe. Prof. Juma aliyasema hayo jana tarehe 18 Mei, 2022 katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi ya Mahakama, Kanda ya Tanga alipokuwa akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Mhe. Kalisti Lazaro ofisini kwake. Katika mazungumzo hayo, Jaji Mkuu ameainisha vipaumbele vinne, ikiwemo idadi ya watu na wingi wa mashauri, vinavyotumiwa na Mahakama ya Tanzania kubaini maeneo ya ujenzi wa miundombinu, hususani Mahakama za Mwanzo na Wilaya.
“Kama mnavyofahamu mwaka huu tutakuwa na sensa ya watu. Kwetu kama Mahakama ni zoezi muhimu sana kwa sababu linatupa mahesabu mapya ya watu na maeneo mbalimbali ambayo yanahitaji huduma. Lengo la sensa ni kusogeza huduma, hivyo tutasubiri matokeo hayo ya sensa ili yatusaidie katika Mkoa huu wa Tanga, kwa mfano, tunapotaka kujenga Mahakama ni sehemu gani ambayo pengine idadi ya watu imeongezeka na sehemu gani ambayo inazalisha mashauri mengi,” amesema.
Jaji Mkuu amebainisha kuwa jana akiwa katika ziara Wilaya ya Kilindi aliambiwa changamoto ya kijiografia ya Wilaya hiyo kuwa haina sehemu ambayo ni katikati ambapo kama ikijengwa Mahakama ya Wilaya sehemu yoyote ile bado itakuwa sehemu mbali na sehemu zingine.
“Kwa hiyo, huo ni mtihani ambao tumeuona. Vile vile tumeuona katika Wilaya ya Handeni. Wilaya ya Handeni ipo karibu kabisa na njia ya kwenda Dar es Salaam na ukilinganisha na makao makuu ya Wilaya bado ni mbali sana. Kwa hiyo sensa ya watu itatusaidia sana katika kupanga upya mpango wetu wa ujenzi wa miundombinu,” amesema Mhe. Prof. Juma.
Amemweleza Mkuu wa Wilaya hiyo kuwa hata zoezi linaloendelea la anuani za makazi ni muhimu kwa sababu Mahakama ingependa kujua anayefungua shauri anaishi wapi, akitakiwa kupelekewa kama wito ifahamike ni wapi na wananchi wanaotaka huduma ziwasilishwe mlangoni kupitia posta itafahamika ni mlango namba ngapi na upo mtaa upi.
“Hivyo zoezi hili ni muhimu sana na ndiyo maana nimewaomba viongozi wa Mahakama kuhakikisha kwamba majengo yetu yanapata anuani. Hatuwezi kuwadai wanaofungua mashauri waonyeshe anuani wakati sisi wenyewe hatuna anuani za makazi,” amesema.
Jaji Mkuu ametaja kipaumbele kingine ambacho huiongoza Mahakama ni maeneo mapya ya utawala. Kwa mujibu wa Mhe. Prof. Juma, kwa bahati mbaya Mahakama imekuwa ikisahauliwa pale Serikali inapoanzisha mikoa na wilaya, wakati mwingine katika maeneo hayo mapya rasilimali inatengwa kujenga vituo vya polisi, lakini mara nyingi huduma za utoaji haki huwa zinasahaulika.
Amebainisha kuwa ukiangalia katika Wilaya 20 ambazo Mahakama za Wilaya zimejengwa ni Wilaya ambazo zilianzishwa bila rasilimali fedha kutengwa kwa ajili ya Mahakama mpya na ndiyo maana zilichelewa kujengwa. Amesema hata zoezi zingine zinazofanywa na Serikali, kwa mfano, kuhamisha watu kutoka Ngorongoro kwenda Wilaya ya Handeni, ni changamoto ambayo itazaa mahitaji ya Mahakama.
“Tunaiomba serikali mapema, mazoezi makubwa kama haya yanapofanyika Mahakama Mwanzo vilevile zijengwe zenye hadhi kuwezesha hata Mahakimu wa Mahakama za Wilaya waweze kutembelea maeneo hayo,” Jaji Mkuu amesema.
Amesema kuwa shughuli za kiuchumi ni kipaumbele kingine kinachotumiwa na Mahakama kujenga miundombinu ya majengo, huku akibainisha kuwa zoezi la sensa litaoMwanzoZa wapi shughuli za kiuchumi zimeongezeka. Aidha, Jaji Mkuu amesema mazingira ya kijiografia vile vile huangaliwa ikizingatiwa kuna maeneo makubwa ambayo yanahitaji usafiri mgumu kufikia maeneo ya utoaji haki.
Katika siku ya tatu ya ziara yake, Jaji Mkuu ametembelea maeneo mbalimbali ya Lushoto na Korogwe. Mbali na kukutana na Wakuu wa Wilaya hizo, Mhe. Prof. Juma ameongea na watumishi wa Mahakama na kupokea taarifa za kiutendaji kutoka kwa Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya hizo.
Jaji Mkuu anatarajia kuhitimisha ziara yake leo Tanga mjini. Mhe. Prof. Juma ameongozana na viongozi mbalimbali kutoka Makao Makuu, wakiwemo Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kevin Mhina, Naibu Msajili kutoka Kurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Malalamiko na Maadili, Mhe. Aidan Mwilapa na Mkurugenzi Msaidizi wa TEHEMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba.
Wengine ni Katibu wa Jaji Mkuu Adrean Kilimi, Mtendaji wa Mahakama Kuu, Masjila Kuu, Bi Maria Itala, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Anatory Kagaruki, mwakilishi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania, Mhe. Nemes Mombury, Mkuu wa Kitengo cha Uhandisi, Bw. Yohana Mashausi, Afisa Utumishi, Bw. Jeofrey Mnemba, Mpima Ramani Abdallah Nalicho, Mhandisi Peter Mrosso na Msaidizi wa Sheria wa Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Hassan Chuka.
Kwa upande wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga yupo Jaji Mfawidhi, Mhe. Latifa Mansoor, Naibu Msajili Beda Nyaki, Mtendaji Humphrey Paya, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga, Mhe. Sofia Masati, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Tanga, Mhe. Ruth Mkusi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi, Mhe. Grace Mwaikono.
No comments:
Post a Comment