Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene, akitoa Hotuba ya Ufunguzi wa Kongamano la Siku ya Familia Duniani, lililoandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na kufanyika jijini Dodoma.
Mwakilishi Mkazi kutoka Shirika la Umaoja wa Mataifa linalohudumia Watoto ( UNICEF), Lawrence Oundo akitoa ujumbe wake wakati wa Kongamano hilo la Siku ya Familia lililofanyika jijini Dodoma.
Na Asha Mwakyonde, Dodoma
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameviagiza vyombo vyote vya Sheria nchini kuhakikisha mashauri yote ya kesi dhidi ya ukatili kwa watoto yanafanyiwa kazi ndani ya miezi sita lengo likiwa ni kuwabaini haraka wanaowafanyia vitendo vya kikatili watoto hao na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Hayo yamesemwa leo Mei 15, jijini hapa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu George Simachawene wakati akizungumza kwa niaba ya waziri mkuu katika kongamano la kitaifa la malezi ya watoto na familia lenye kauli mbiu isemayo "Dumisha Amani na Upendo kwa Familia Imara: Jitokeze kuhesabiwa waziri huyo amesema mahauri yanayohusu ukatili dhidi ya watoto yasitelekezwe na badala yake yafanyiwe kazi haraka iwezekanavyo.
Ameaema mashauri ya ukatili, mauaji ya vikongwe yanafanyiwa kazi wakati umefika sasa mashauri yote yanayohusu kesi za ukatili dhidi ya watototo yafanyiwe kazi haraka.
Waziri huyo amezitaja takwimu za ukatili mwaka 2021 kuanzia mwezi Januari hadi Desemba zinaonyesha jumla matukio 11,499 ya ukatili dhidi ya watoto na matukio makubwa yalioongoza ni ubakaji 5899, mimba 1977 na ulawiti 1114.
Aidha amewataka watoto wote kutoogopa kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa vitendo hivyo vya ukatili iwe kwa walimu au kwa mtu yoyote aneyemuamini kwani hali inaonyesha matukio mengi ya kikatili hutokea katika ngazi ya familia wakiwemo walezi ndugu na hata wazazi.
‘’Msirubuniwe na kuendelea kuficha siri mtaharibikiwa na ndoto zenu zitapotea kama umefanyiwa ukatili toa taarifa kwa mtu utakayeona anaweza kukupa msaada wa haraka,’’amesema Simbachawene.
Amewataka wazazi na walezi wenye tabia ya kumalizana nyumbani kesi dhidi ya ukatili wa watoto kuacha mara moja na kwamba atatakayebainika afikishwe katika vyombo vya sheria bila kujali ndungu, baba au mjomba kwa ukatili huo.
Awali akizungumza katika kongamano hilo Waziri Maendeleo ya Jamii ,Jinsia , Wanawake na Makundi Maalum Dk. Dorothy Gwajima amesema kupitia wizara wizara hiyo inatambua na inathamini familia kama chanzo cha nguvu kazi ya Taifa hivyo katika kuimarisha uwezo wa familia kutimiza majukumu yake.
Amesema wizara hiyo imekuwa ikitekekeza afua mbalimbali za kuwezesha familia kuishi kwa amani na Upendo na baadhi ya afua hizo ni kutoa elimu ya malezi chanya kwa Wataalamu wa Halmashauri 7,445 wakiwamo maafisa wa maendeleo ya jamii, Ustawi wa jamii na maafisha lishe na walimu.
" Wataay hawa kwa kipindi cha Julai 2020 hadi Juni 2021 walifanikiwa kutoa mafunzo ya wazazi na walezi vinara (Champions),110,805 ambao wamepewa jukumu la kuendeleza elimu ya malezi kwa wenzio wao katika mikoa 26 ya Tanzania Bara," amesema Dk. Gwajima.
Dk. Gwajima ameeleza kuwa katika kuhakikisha wazazi wote hasa wanaume wanashirikiana kikamilifu katika ya watoto na kwamba wizara hiyo imeandaa Mwongozo wa Taifa wa Wajibu wa Malezi na Walezi katika malezi ya familia umeandaliwa kwa ajili ya kutoa elimu kwa jamii inayolenga kwa watoto kuanzia umri wa miaka 0 hadi 18.
Naye Mwakilishi Mkazi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF), Lawrence Oundo amesema kuwa mtoto wa kiume na wakike wanahaki ya kupata malezi sawa hivyo wazazi wanapaswa kuwalinda dhidi ukatili.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la ICS Kudely Joram amesema kuwa wanaendelea kufanya kazi ya kuhakikisha ulinzi na usalama wa mtoto unaimarika ndani na nje ya shule.
"Tunashirikiana na serikali katika masula ya malezi ya watoto, tunaishukuru serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwani tunaona hata wanaume sasa sauti zao za ukatili zimeanza kusikika," amesema Mkurugenzi huyo wa ICS.
Kwa upande wake mwalimu Doris Sawali kutoka shule ya sekondari wilaya ya hai Kilimanjaro amewataka wazazi kuwa karibu na watoto kwani matukio mengi wanafunzi wamekuwa wakitoa taarifa kwa walimu.
No comments:
Post a Comment