HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 21, 2022

Dola mil. 425 kuboresha elimu ya juu miaka mitano

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza baada ya utiwaji saini wa mikataba hiyo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga akizungumza kwenye uzinduzi huo.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Francis Michael akizungumza kabla ya kusaini mikataba hiyo na wakuu mbalimbali wa vyuo na taasisi zitakazoshiriki kwenye mradi wa HEET.


Na Irene Mark

BENKI ya Dunia imeikopesha Tanzania Dola milioni 425 za Marekani kwa ajili ya kuchochea mageuzi ya kiuchumi kwenye sekta ya elimu hasa elimu ya juu, ndani na nje ya nchi.

Fedha hizo zinaendesha Mradi wa Mageuzi ya Sekta ya Elimu kwa ajili ya Kuchochea Uchumi (HEET PROJECT) kwa miaka mitano.

Mradi huo utavinufaisha vyuo vikuu 14; Taasisi tatu zilizopo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Taknolojia ambazo ni Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimunya Juu, Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na vyuo vitano vilivyo chini ya Wizara ya Fedha.

Akizungumza muda mfupi kabla ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Francis Michael, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Omari Kipanga, amesema mradi huo utaboresha sekta ya elimu ya juu kuanzia ubora wa wahadhiri na miundombinu

Naibu Waziri Kipanga amewataka wasimamizi wa mradi huo wa HEET kuhakikisha utekelezaji wake unaleta tija inayokusudiwa huki akiwasisitiza kuwasiliana kwa kila hatua wakati wa utendaji wao.

“HEET Project inataka wahadhiri kuongeza viwango vyao vya elimu, kupitia mradi huu mwenye digrii moja akasome apate ya pili, mwenye digrii mbili aongeze ya tatu... yaani iwe hivyo hadi tupate maprofesa.

“Sio hivyo tu mradi huu wa miaka mitano utasogeza kampasi ya vyuo kwenye mikoa mingine 17 hapa nchini ambayo haina vyuo  hivyo na kipekee zaidi mradi huu utajenga chuo kikuu kipya cha Tehama,” amesema Naibu Waziri Kipanga.

Ameitaja mikoa 17 itakayonufaika kuwa ni Lindi ambapo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitajenga tawi jipya huko, Ruvuma, Songwe, Rukwa, Simiyu, Kigoma, Tabora, Shinyanga, Singida, Dodoma, Kagera, Mwanza, Tanga, Manyara, Katavi, Mara na Pwani.

Ameeleza eneo jingine la utekelezaji wa bajeti hiyo kuwa kuwezesha uwepo wa vifaa wezeshi vya kujifunzia na kufundisha ili kupata wahitimu bora waliotoka kwenye mikono ya wahadhari mahiri.

Naibu Waziri Kipanga, aliwataka watendaji wa mradi huo kuhahakisha wanatengeneza kamati maalum ya ufuatiliaji na tathimini ya mradi kwa kila hatua.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Michael amesema  mradi huo utasaidia kupambana na changamoto za elimu hususan elimu ya juu nchini.

"Kitendo cha leo kusaini mkataba huu na wakuu wa vyuo vyote na taasisi zitakazoshiriki kwenye utekelezaji wa mradi huu kitaharakisha ukamilifu wake na ufanisi,” amesema Katibu Mkuu Michael.

Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia hapa Tanzania, Nkahiga Kaboko, amesema ni furaha ya ofisi yake kuona sekta ya elimu hapa nchini inakuwa bora hivyo ameahidi kuendeleza ushirikiano zaidi kwenye elimu.

“Nasisi Benki ya Dunia tutafanya uzinduzi wetu titawakaribisha waandishi wa habari kuhusu hili na tutalifafanua zaidi... leo sio siku yetu ila nawashukuru kwa kutualika tushuhudie mnavyosaini.

“Nawapongeza sana wakuu wote wa vyuo na taasisi zinazoshiriki kwenye mradi huu, timu zote zitakazofanyakazi kwenye mradi huu nawatakia mafanikio mema asanteni sana Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,” amesema Koboko.

Akizungumzia mradi huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema mkopo huo ni matokeo ya ziara za kikazi anazofanya Rais Samia Suluhu Hassan nje ya nje hivyo tunamshukuru sana mheshimiwa Rais Samia.

“Nilikuwa Zanzibar nikawaomba mvutevute kidogo ili nami nishiriki na kuwaonesha wenzetu wa Benki ya Dunia kwamba jambo hili ni muhimu sana kwetu licha ya kuwa leo ni Jumapili lakini timu nzima ya wizara ipo hapa,” amesema Profesa Mkenda.

No comments:

Post a Comment

Pages