HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 08, 2022

HIYO NDIYO NDOTO YANGU


Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.  

 

Adeladius Makwega-DODOMA 

 

Mara baada ya Jakaya Kikwete kuwa Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005 miongoni mabadiliko makubwa aliyoyafanya mwaka 2008/2009 ni kuzirudisha shule za sekondari TAMISEMI.

 

Kwa nini alifanya hivyo? Mtumishi ambaye ni mwalimu anayefundisha Isimani sekondari Iringa vijijini wakati huo, mwalimu anayefundisha Ndanda sekondari au yule anayesomesha Rugambwa sekondari wote waliwajibika kwenda Magogoni Dar es Salaam kufuatilia uhamisho, posho ya kujikimu, kupanda madaraja na mengine mengi.

 

Kusudio hilo liikuwa na nia njema kuwapunguzia gharama, kero na urasimu watumishi na wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tangu hapo wakawa wanayafuatilia hayo kwa Wakurugenzi wa Majiji, Miji, Manispaa na Wilaya.

 

Kwa nini ninayaandika haya siku ya leo? Juni 6, 2022 nikiwa njia panda ya Mji wa Serikali nilikutana na dada mmoja mmoja, mrefu, mweupe analia. Kibinadamu nilimuuliza boda boda mbona dada huyu huyu uliyemshusha analia? Alijibu kuwa yeye amemchukua kutoka TAMISEMI akiwa analia, hafahamu lililomkuta

 

Kibinadamu tu nikamsogelea, nikamsalimia, nikamwambia pole sana ! Akasema asante. Nikamuuliza mbona kilio, una msiba? Alinijibu, akasema afadhali ingekuwa msiba.Ningezika yangekwisha,lakini haya wala hayamaliziki.

 

”Mimi ni mtumishi wa halmashauri, nafuatilia uhamisho, nimegomewa.”

 

Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, yupo likizo ya kujifungua, aliyekaimisha (RAS) alishindwa kunisaidia, alivyogoma mkurugenzi wangu ndiyo nikarudi TAMISEMI kuwaeleza ili wanisaidie.

 

Alipofika TAMISEMI alipokelewa na watumishi wa mapokezi na kuelekezwa ofisi nambari 44, hapo alijitambulisha kuwa alishafika ofisi hiyo mara nyingi, pia hata mtumishi wa TAMISEMI aliyempokea, alimkumbuka kwa kusema haya:

 

“Kama sura yako ninaikumbuka, leo una shida gani?” Nilisimuliwa.

 

Mkurugenzi kagoma na RAS yupo likizo ya kujifungua. Huku akionesha eneo la tumbo lake ambalo amefanyiwa upasuaji. Afisa wa TAMISEMI wa ofisi nambari 44, ambaye niliambiwa ni mtumishi hodari sana mithili wa watumishi wa benki, alielekeza aende ofisi nambari 20 hapo hapo TAMISEMI Mji wa Serikali.

 

Alipofika ofisi nambari 20 saa 5.39 asubuhi, alipokelewa na makarani wawili bibi na bwana alijieleza na kuambiwa akae katika makochi jirani na mlango wa kuingia kwa mkubwa wa ofisi hiyo.

 

Akiwa hapo walifika wageni wawili ambao walijitambulisha kuwa ni Mbunge na Mwenyekiti wa Halimshauri ya Ndanda, walipojitambulisha waliruhusiwa kumuona mkubwa wa ofisi nambari 20.

 

Alikaa katika makochi hayo kwa saa mbili, huku kukiwa kimya, bila majibu yoyote yale. Saa saba mchana akaambiwa kuwa akakae katika viti vya nje vya ofisi hiyo ambapo kulikuwa na wageni wengine.

 

Akiwa nje, wale waheshimiwa kutoka Ndanda walitoka na kwenda zao. Alikaa hapo kwa saa moja na nusu. Walinzi wa ofisi hii wakamfuata, wakamwambia kuwa dada jitahidi kuwakumbusha, pengine watakuwa wamekusahau. Alistuka, akaamua kurudi kwa makarani wa ofisi nambari 20.“Jamani naombeni nimuone huyu mkubwa, anisikilize.” Wale makarani walijibu kuwa:“Ehee kumbe bado upo! Endelea kusubiri tu, amesema kuwa kwa sasa asiingie mtu.”

 

Akiwa hapo alitoka mama mmoja ndani ya chumba nambari 20. Makarani wale wakamuuliza ehee bosi utarudi?

 

“Ninaweza kurudi.”Alijibu.

Muda huo ni saa 9.30 Alasiri, aliambiwa rudi ofisi nambari 44. Alipofika huko hii ilikuwa ile ofisi ya maafisa hodari hapo walimuelekeza aende ofisi nambari 43.

 

“Kama una malalamiko yako, mwaandikie barua Katibu Mkuu TAMISEMI.” Alijibiwa baba mmoja na huku mama mwenye lugha kavu, mkali akisema kuwa kama umeshindwa kusaidiwa huko, hapa hakuna chako.

 

“Hapa, hata kama unalia vipi, sisi tumezoea kuwaona watu kama wewe kila siku, na usitusumbue kabisa. Mnatoka huko na makosa yenu, mnakuja kutusumbua tu. Kama Mkurugenzi wako kashindwa kukusaidia na RAS wako pia. unataka mimi nifanye nini?” Alisema Afisa Mwanamke wa ofisi nambari 43.

 

Hapo hapo ndipo alitoka TAMISEMI huku akilia na kupanda bodaboda na mimi kukutana naye majira ya 10.35 jioni kituo cha basi la Mtumba.

 

Msomaji wangu kwa hakika umeelewa kilichotokea, naomba kwa hisani yako niyaseme mambo haya:

 

Huyu mkubwa wa ofisi nambari 20 TAMISEMI aliyeondoka ofisini saa 9.30 alasiri aliyejibu -ninaweza kurudi alipaswa kuwasikiliza wageni wote wanaofika ofisini kwake, siyo wale wakubwa wa Ndanda tu.

 

Kama mtumishi umma ana wageni wengi ndani ya geti la ofisi yake anapaswa kuwahudumia hadi mgeni wa mwisho aliye ndani ya jengo hilo, hata ikifika saa mbili ya usiku. Kwa zile saa za ziada, kwa mwongozo wa malipo atalipwa posho ya kazi za ziada (Extral Duty Allowance-EDA).

 

Makarani hawa wawili wa ofisi nambari 20 wao mara nyingi ni wapokea maagizo tu, hawana kosa lolote lile, makarani hawa tukiwananga tunawaonea tu.

 

Kwa yule afisa mama wa ofisi nambari 43 ajitahidi sana kuwapokea wanaofika hapo kwa moyo wa unyenyekevu, upole na wema. Hizi kazi za umma ni za muda tu, akumbuke kuwa hata nduguze huko walipo nao wanahudumiwa na watumishi wengine wa Tanzania hii hii.

Katika utumishi wa umma kila mmoja ataondoka tu, iwe kwa kustaafu, kuachishwa, kuacha mwenyewe,ugonjwa  na hata kufariki dunia,kwa hakika hayupo anayeweza kudumu milele katika utumishi wa umma.

 

Walinzi wa TAMISEMI walimwambia yule dada:

 

“Angalia wasikusahau”

 

Tafsiri yake kuwa hapo TAMISEMI wageni wanasahaulika.Walinzi hao ni Watanzania kama mimi na wewe na wanayoyasema ni yale yanayoonekana, wanayasema hayo kuwasaidia nduguzo Watanzania na wanyonge wenzao.Kwa hakika pengine wanaona vihoja vingi hapo.

 

Naiweka kalamu yangu chini ili kuwakumbusha TAMISEMI kuwa dhamira ya Rais wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete ya kuzipeleka baadhi idara hapo nia ni kuboresha na kusogeza huduma jirani na wananchi na siyo vinginevyo.

 

Kinyume chake basi  idara ya Afya irudi Wizara ya Afya, Elimu Sekondari irudi Wizara ya Elimu, Mifugo Irudi Wizara Mifugo na Idara ya Kilimo Irudi Kilimo, maana yake TAMISEMI haipo, hilo siyo kusudio la serikali yetu.

 

Utumishi wa umma unapaswa kuiga namna watumishi wa benki zetu wanavyofanya kazi na kuwasikiliza wateja wao, siyo kwamba watumishi wa benki wanalipwa pesa nyingi kuliko watumishi wa umma. Binafsi nina imani wapo watumishi wa umma wengi wanalipwa mishahara naposho nyingi zaidi ya watumishi wa benki, bali hilo ni namna benki zilivyojiwekea utaratibu huo wa kutoa huduma tu, hiyo ndiyo ndoto yangu.

 

makwadeladius@gmail.com

 

0717649257

 

No comments:

Post a Comment

Pages