HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 30, 2022

Mdahalo Kumbukizi ya Hayati Mkapa kufanyika Zanzibar


 

NA TATU MOHAMED 

ZAIDI watu 500 wanatarajiwa kushiriki mdahalo maalum uliyoandaliwa na taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation (BMF) kwa kushirikiana na Serikali kama sehemu ya kumbukizi ya hayati Mkapa.

Mdahalo huo utakuwa wa siku mbili ambapo unatarajiwa kufanyika Visiwani Zanzibar huku ukinguliwa na Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Othman Masoud na kufungwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa BMF, Dk. Ellen Senkoro wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya mdahalo huo unaotarajiwa kufanyika Julai 13 hadi 14 mwaka huu visiwani Zanzibar. 

"Kumbukizi ya Rais hayati Mkapa inafanyika ikiwa na kauli mbiu 'uongozi madhubuti hamasa ya mabadiliko kwa wote', kwa siku hizo mbili washiriki hao watapata fursa ya kujadili mada kuu mbili ikiwemo ya namna ya kuongeza kasi katika mikakati ya mabadiliko kwenye mifumo ya afya Tanzania kupitia biashara ushirika.


"Viongozi wengine wa kitaifa watakaohudhuria mdahalo huu ni pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi, Viongozi wakuu wa Serikali,  marais na viongozi wastaafu kutoka Tanzania Bara na visiwani," amesema.


Ameongeza kuwa, viongozi wengine ni mabalozi wanaowakikisha nchi zao hapa nchini, wakuu wa mashirika ya kimataifa hapa nchini, asqsi za kiraia, viongozi wa dini, wakuu wa taasisi mbalimbali za sekta binafsi na umma, wanafamilia pamoja na marafiki wa hayati Mkapa kutoka ndani na nje ya nchi,".

Hata hivyo amesema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi ameteuliwa kuwa msarifu wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa Foundation (BMF) akilithiri mikoba  hayati Benjamin Mkapa ambaye ndiye alikuwa akishika nafasi hiyo mpaka pale umauti ulipomkuta. 

Dk. Senkoro amesema Rais Mwinyi ameanza kushika nafasi hiyo Desemba mwaka jana na wanaamini ataweza kuendeleza maoni ya mwanzilishi wa taasisi hii.

Amesema moja ya majukumu ya msarifu ni kuteua wajumbe wa bodi ya taasisi hiyo na kuhakikisha anashirikiana na bodi hiyo kutafuta fedha za kuendeleza taasisi.

"Katiba iliyoanzisha hii taasisi miaka 16 iliyopita ilitambua kuwa kuna mwanzilishi alafu kuna msarifu ambaye awali alikuwa Hayati Mkapa kwahiyo alipofariki kwa mujibu wa katiba ilikuwa lazima kumtafuta mrithi wake na uzuri katiba yetu inatambua hilo siku msarifi hayupo upo mchakato unapaswa kufanyika kumpata mwingine.


"Ulikuwa ni mchakapo wa muda mrefu na hatimaye tumefanikiwa kumpata mrithi wake ambaye ni Rais Mwinyi, kihistoria ndiye alikuwa Mwenyekiti wa kwanza wa bodi ya wadhamini ya taasisi hii wakati ule ilipoanzishwa," amesema.

Naye Meneja Tathimini na ufatiliaji wa miradi ya taasisi, Rahma Musoke amesema taasisi hiyo katika kuboresha huduma za afya kupitia wadau wa maendeleo wamefanikiwa kuwaajiri watumishi 10042 wa afya ambao wamepelekwa katika vituo mbalimbali ili kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Amesema kupitia miradi yake mingine taasisi imefanikiwa kujenga nyumba 482 za watumishi wa afya katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo yale ambayo ni magumu kufikika.

No comments:

Post a Comment

Pages