Postamasta
Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo (kulia) na Mkurugenzi wa
Kampuni ya Tutume, Misana Manyama, wakisaini makubaliano ya biashara ya
usafirishaji wa sampuli za kibaiolojia jijini Dar es Salaam.
PostaMasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo akizungumza wakati wa utiaji saini makubaliano ya biashara ya usafirishaji wa sampuli za kibaiolojia kati ya Shirika hilo na Kampuni ya TUTUME.
Shirika la Posta Tanzania na Kampuni ya usafirishaji TUTUME wameingia makubaliano ya biashara ya usafirishaji wa sampuli za kibaiolojia kwa lengo la kuongeza tija na mapato ya shirika, serikali na kumpatia mwananchi huduma bora.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wa utiaji saini huo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema makubaliano hayo yataliongezea wigo shirika hilo la utoaji wa huduma kwa jamii.
"Ushirikiano huo kati ya Shirika la Posta Tanzania na Tutume ni wa manufaa kwa pande zote mbili kwani utaongeza wigo wa utoaji huduma kwa jamii na viwango vya ubora na utoaji huduma yaani quality of service standards” amesema
Waziri Nape amesema ushirikiano huu pia utasaidia kuongeza malengo ya Serikali ya kuimarisha huduma za afya mpaka vijijini kwani ni wazi kuwa taasisi hizo mbili zitapata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika kuwahudumia wananchi kwa kuwa sehemu ya usafirishaji wa sampuli za damu.
"Kupitia makubaliano haya Shirika la Posta Tanzania litahakikisha sampuli hizo zinafikishwa zinapotakiwa kufika na kazi hii inayofanywa kwa ushirikiano na TUTUME itaongeza kasi ya kuwafikia wananchi wengi zaidi katika maeneo mbalimbali," amesema
.Hata hivyo Waziri Nape amelitaka shirika hilo la Posta Tanzania kutumia fursa hiyo ya uwekezaji kwenye kilimo hasa katika kusafirisha vitu mbalimbali ikiweno mbegu.
“Serikali tumewekeza sana kwenye sekta ya kilimo, licha ya kushuhudia tukio hili kubwa ambalo linaenda kufanya mageuzi kwenye sekta ya afya lakini ni matumaini yangu kwamba posta mtatumia fursa hii ya uwekezaji kwenye kilimo, tutashuhudia mashirikiano ya posta na sekta ya kilimo katika kusafirisha vitu mbalimbali ikiwemo mbegu na sampuli mbalimbali” amesema
Vilevile Waziri Nape amesema lengo la Serikali ya awamu ya sita iliyopo chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi hivyo jitihada zinazofanywa na shirika hilo zinaungwa mkono.
Naye PostaMasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo amesema katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya zikiwemo za uchunguzi, serikali kupitia Wizara ya afya imelipa jukumu shirika hilo la kusafirisha sampuli za maabara kutoka vituo vya afya kwenda maabara za uchunguzi na kurejesha majibu yake baada ya uchunguzi kufanyika.
Amesema kuwa sampuli zinazosafirishwa ni zile zinazotokana na magonjwa ya kawaida kama vile kifua kikuu, HIV pamoja na magonjwa ya mlipuko kama vile UVIKO-19.
Mbodo amesema ili kuongeza ufanisi na ubora wa usafirishaji wa sampuli hizo za maabara na majibu yake kwa wananchi, waliona ni vyema waingie makubaliano ya ushirikiano katika usafirishaji wa sampuli hizo na kampuni ya usafirishaji ya TUTUME ambayo imewahi kujishughulisha na usafirishaji wa sampuli za maabara.
"Usafirishaji wa sampuli hizo umegawanyika katika sehemu kuu mbili, ya kwanza ni kutoka katika vituo vya afya ngazi ya kwanza vinavyotumika kukusanya sampuli kutoka kwa wananchi kwenda katika vituo vya afya ngazi ya pili zinazotumika kuhifadhi na kuchakata sampuli.
"Sehemu ya pili ni kutoka katika vituo vya afya ngazi ya pili kwenda kwenye maabara kwa ajili ya uchunguzi na baada ya zoezi hilo majibu yake yanarudishwa kwa wananchi husika," amesema
Mbodo amesema ili kuongeza ufanisi na ubora wa usafirishaji wa sampuli hizo kutoka maabara na kurejesha majibu kwa wananchi, waliona ni bora kuingia makubaliano ya ushirikiano na TUTUME katika usafirishaji wa sampuli.
"Makubaliano ya ushirikiano wetu niya kiwakala ambapo TUTUME wanakwenda kuwa wakala wa Shirika la Posta Tanzania katika usafirishaji wa sampuli za maabara na majibu yake kutoka vituo vya afya ngazi ya kwanza kwenda ngazi ya pili nchi nzima, wakati Shirika la Posta likiendelea na usafirishaji wa sampuli hizo za maabara na majibu yake kutoka katika vituo vya afya ngazi ya pili kwenda maabara ya uchunguzi kote nchini," amesema na kuongeza
"Kupitia ushirikiano huu pamoja na shirika kuongeza mapato ila tunakwenda kuongeza ajira kwa vijana wetu wa bodaboda ambao kwa sasa wapo 450, ajira zitaongezeka mara tatu kwani hawa ndio watakuwa wakitumika kusafirisha sampuli hizi," amesema
Amesema shirika hilo limejipanga kikamilifu kuhakikisha wanasimama kikamilifu utekelezaji wa kazi hiyo ili wananchi wapate huduma za afya bora na uhakika.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TUTUME, Misana Manyama amewahakikishia wananchi kuwa fursa hiyo waliyopewa na serikali kupitia shirika la Posta wataitumia kikamilifu kwa kuwa wanauwezo wa kufanya kazi hiyo kwa ubora.
"Tutaifanya kazi hii kwa ukamilifu kabisa kwasababu tumeshaifanya kwa kipindi cha nyuma na tunaendelea kuifanya sawasawa, hivyo Shirika la Posta limetuamini na hatutawaangusha, titayatekeleza yale yote yaliyopo kwenye mkataba," amesema
No comments:
Post a Comment