HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 30, 2022

NMB yashiriki Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Wafanyakazi wenye Ulemavu


 Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay akiwasilisha mada kwenye Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Wafanyakazi wenye ulemavu nchini uliofanyika Jijini Dodoma.

 

SABABU kuu tatu zimetajwa kuwa changamoto ya kuwakosesha ajira watu wenye ulemavu nchini licha ya kuwa wanakuwa na sifa zinazotastahili.

Sababu hizo zilitolewa Jijini Dodoma na Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay kwenye Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa wafanyakazi wenye ulemavu ulioitishwa na taasisi ya Ikupa Trust huku NMB wakiwa moja ya wadhamini.

Akonaay alitoa kauli hiyo alipozungumza kwa niaba ya waajiri juu ya changamoto wanazokutana nazo wakati wa kuajiri kwani watu wenye ulemavu huwa wachache ingawa alisema ndani ya NMB watu wenye ulemavu wapo.

Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay alizitaja baadhi ya changamoto hizo ni kutojiamini hivyo kushindwa kutuma maombi ya kazi.


Nyingine ni watu wenye ulemavu kutokuwa na ari ya kujitolea na kukosekana kwa kanzi data ya wenye ulemavu ili kuwatambua katika uwezo wao.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira,Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, aliziomba taasisi za fedha kuendelea kuwaamini wenye ulemavu na kutimiza matakwa yao, si kwa kuomba bali kwa haki.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Ikupa Trust, Stella Ikupa alisema kundi hilo linakutana na changamoto nyingi lakini wanalilia utekelezaji wa sheria ambayo inasema kila walipo watumishi 20, lazima asilimia tatu yao iwe ni wenye ulemavu.

Ikupa alisema tatizo la miundombinu ni kubwa hasa katika majengo ya Serikali ikiwemo vyoo ambapo huwafanya baadhi ya wenye ulemavu kulazimika kushinda njaa au kutokunywa maji kutwa nzima wakiwepo kazini wakiogopa kwenda vyooni kwani mazingira si rafiki.

Kwa upande mwingine Ikupa alizishukuru taasisi za fedha ikiwemo NMB kwamba wamekuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia wenye ulemavu ikiwemo Taasisi ya Ikupa Trust.

No comments:

Post a Comment

Pages