HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 30, 2022

TEF, wanahabari waungana kuhakikisha sheria kandamizi zinaondolewa makali

NA MWANDISHI WETU

 

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile ameungana na wanahabari kuhakikisha kuwa sheria zinazoumiza wanahabari zinaondolewa makali.

 

Hata hivyo TEF imefafanua kuwa chombo hicho kitaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo serikali kuwepo kwa mazingira rafiki kwa wanahabari kutekeleza majukumu yao.

 

Kauli ya Balile imekuja wakati ambapo wadau mbalimbali wa sekta ya habari wakipendekeza kufanyika kwa marekebisho  katika Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya Makosa Mtandaoni ya mwaka 2015.

 

Akizungumza kwenye semina na wanahabari,jijini Dar es Salaam,Balile amesema wameungana kwa pamoja katika kuhakikisha wanaweka mazingira rafiki kwa wanahabari kufanya kazi zao.

 

“Kuna sheria nyingi zilizowekwa na kulenga waandishi ama kushambulia tasnia, tumeungana kwa pamoja kuhakikisha sheria hizo zinaondolewa makali yanayoumiuza wanahabari.

 

“Ni bahati nzuri sasa serikali nayo imeliona hili, mwelekeo wetu una matumaini lakini tunapaswa kuendelea kuwa pamoja mpaka tunafikia lengo,” amesema Balile.

 

Hata hivyo Kifungu cha 7 (2) (b) cha sheria ya Huduma ya Habari ya Mwaka 2016, inaingilia moja kwa moja uhuru wa mhariri katika kutoa ama kuchapisha habari.

 

Akitoa ufafanuzi juu ya vifungu katika sheria hiyo, Wakili wa kujitegemea na Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA-TAN) James Marenga, amebainisha kuwa kifungu cha 7 (2) (b) cha sheria hiyo kinapoka mamlaka ya mhariri katika kuamua habari gani ya kuchapishwa.

 

“Kifungu cha 7 (2) (b) (iv)  cha Sheria ya Huduma za Habari,  kinatoa maelekezo kwa vyombo vya habari binafsi kuchapisha habari zenye umuhimu kwa taifa kwa maelekezo ya Serikali.

 

Marenga ameongeza kuwa Kifungu hicho cha Sheria kinaingilia uhuru wa uhariri na hasa kwenye vyombo vya habari vya binafsi.

 

“Kifungu hiki kidogo hakiwezi kufanyiwa marekebisho, tunapendekeza kifutwe”

 

“Mapendekezo yanakusudia kuwezesha maamuzi ya kihariri kuzingatia vigezo vya taaluma bila kuathiriwa na maamrisho yasiyo ya kitaaluma. Uhuru wa uhariri (editorial independence) utalindwa”amesema Marenga.

 

Marenga amebainisha kuwa Kifungu cha 7 (3), (a), (b), (c), (f), (g), (h), (i) na (j) vya Sheria hiyo, vinatoa udhibiti wa aina fulani ya habari ama maudhui.

 

“Mamlaka hii ya kisheria inatoa mwanya kwa serikali kudhibiti taarifa zinazotolewa na vyombo binafsi vya habari.

 

“Kifungu hiki na vifungu vyake vidogo vinakiuka uhuru wa wa kujieleza bila ya kuwa na sababu za msingi. Hii pia ni kwa mujibu wa maamuzi ya Mahakama ya Haki ya Afrika ya Mashariki (EACJ)”amesema Marenga.

 

Wadau wa habari wanapendekeza kifungu hicho na vifungu vyake vidogo vifutwe kama ilivyoamuliwa na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki. (EACJ).

No comments:

Post a Comment

Pages