HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 22, 2022

RAIS Samia azidi kupongezwa

 


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, kizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM jijini Dodoma.


 Na Jasmine Shamwepu, Dodoma

HALMASHAURI Kuu ya Taifa imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa ukomavu, ustahimilivu, uhodari na dhamira yake njema ya kufanya maridhiano na vyama vya siasa nchini lengo likiwa ni kuimarisha umoja, ushirikiano, mshikamano, amani na utulivu kwa maendeleo na ustawi wa watanzania wote.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa
Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa baada ya kumallizika kwa kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dodoma.

Shaka alisema Halmashauri kuu ya Taifa imevipongeza vyama vyote vya siasa kwa kukubali kuunga mkono hatua hiyo ya Maridhiano na kuwa wamoja katika nyanja ya kusiasa.

Aidha alisema kutokana na maridhiano hayo kwa vyama vya siasa Chama Mapinduzi CCM kimeishauri serikali kuharakisha utekelezaji wa masuala yote yatakayojenga kuaminiana, kuimarisha ushirikiano na umoja wa kitaifa kwa ustawi wa wananchi wote.

"Miongoni mwa mambo ambayo Halmashauri Kuu imeshauri kutazamwa ni pamoja na kesi zenye sura ya kisiasa kwa wafuasi na wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa nchini na ikiwezekana zimalizwe haraka," alisema Shaka.

Pia alisema Chama kimeishauri serikali utekelezaji wa masuala yote ya kuimarisha demokrasia nchini na mazingira ya kisiasa yafanyike bila kuathiri uhuru na usalama wa nchi yetu.

PONGEZI KWA DKT HUSEIN MWINYI

Vilevile  alisema Halmashauri Kuu ya Taifa imempongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt Husein Ali Mwinyi kwa kuendelea kuonesha uvumilivu na ukomavu wa kiuongozi katika kuongoza serikali ya umoja wa kitaifa hali inayochochea umoja, amani na utulivu kwa wananchi wa Zanzibar na hivyo kuharakisha maendeleo yao.

KATIBA MPYA

Alisema Halmashauri Kuu ya Taifa kwa kauli moja imekubaliana kuwa kuhusu upatikanaji wa Katiba Mpya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinakubaliana na umuhimu wa kupatikana kwa katiba mpya kwa kuzingatia mazingira ya sasa na hivyo kinaishauri serikali kuona namna bora ya kufufua, kukwamua na kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya kwa maslahi mapana ya Taifa na Maendeleo ya watanzania wote.


UCHAGUZI NDANI YA CHAMA

Alibainisha kywa ,Halmashauri Kuu ya Taifa imepokea na kuridhishwa taarifa ya maendeleo ya uchaguzi mkuu wa ndani ya Chama ambao umeshakamilika kwa asilimia 99.5 katika ngazi ya mashina na matawi kote nchini na sasa upo katika ngazi ya Kata/Wadi. Chama kimetakiwa kuzifanyia kazi kasoro zilizojitokeza katika ngazi hizi ili kuimarisha ushiriki wa haki, usawa na demokrasia katika ngazi zote zinazofuata kwa mujibu wa kalenda ya uchaguzi ya Chama.

UCHAGUZI WA KUJAZA NAFASI ZA WAJUMBE WAWILI WA KAMATI KUU YA HALMASHAURI KUU YA TAIFA YA CHAMA CHA MAPINDUZI.

Alisema Halmashauri Kuu ya Taifa imefanya uchaguzi wa kujaza nafasi mbili za wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri ya Taifa zilizokuwa wazi kwa kuwachagua kwa kura Ndugu Stephen Masatu Wassira na Ndugu Theresia Adriano Mtewele.

UTEUZI WA WENYEVITI WA HALMASHAURI ZA WILAYA NA MAMEYA

Alisema Pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imefanya uteuzi wa wenyeviti wa halmashauri za wilaya na Mameya kama ifuatavyo:-

Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Mji
 Ndg Erasto B. Mpete

Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro
Ndg Mohamed Festo Bayo

Halmashauri ya Manispaa ya Moshi
1. Ndg Stuart Nathaniel Nkinda
2. Ndg Apaikunda Ayo Naburi
3. Ndg Zuberi Abdallah Kidumo

No comments:

Post a Comment

Pages