Na Mwandishi Wetu
BENKI ya CRDB Plc (DSE: CRDB) kwa kushirikiana na Mfuko wa Uwekezaji wa Norway kwa Nchi Zinazoendelea (Norfund) na Mfuko wa Uwekezaji wa Denmark kwa Nchi Zinazoendelea (IFU) kuwekeza nchini Congo.
Uwekezaji wa CRDB ni Dola milioni 30 za Marekani una lengo la kuchichimua uchumi wa nchi ya Jamuhuri ya Watu wa Congo (DRC), huku ikidhamiria kutekeleza mkakati wa upanuzi wa benki hiyo katika soko kubwa la Afrika Mashariki na Kati.
Maskani ya Kampuni tanzu ya DRC itakayokuwa na makao yake katika kitovu cha kibiashara cha mji wa Lubumbashi, itaanza hivi karibuni baada ya kuidhinishwa na Benki Kuu ya Tanzania tangu Mei, 2021.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema hayo mwanzoni mwa wiki hii na kufafanua kwamba uongozi wa benki yake imeiona DRC kuwa ni soko la kusisimua linalotoa fursa ya kipekee kwa kundi kubwa kubadilisha maisha nje ya mipaka ya Tanzania.
“Benki ya CRDB imepata washirika wawili wa hisa ambao ni Norfund na IFU kwa uwiano wa CRDB kumiliki hisa za asilimia 55 na hawa wawili watagawana asilimia 22.5 ya hisa kila mmoja," alisema Nsekela.
Alisema IFU inawekeza katika makampuni yenye uwezo wa kifedha na kuchangia katika mabadiliko ya kijani kibichi na pia kujenga jamii zenye haki na jumuishi.
Alifafanua kwamba Norfund inatoa kipaumbele kwa uwekezaji katika maeneo manne ya uwekezaji yanayowiana na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.
“Maeneo hayo ni nishati safi, taasisi za kifedha, miundombinu ya kijani kibichi na biashara zinazoweza kuongezeka,” alisema Nsekela.
Makamu wa Rais wa Norfund, Espen Froyn alisema amefurahishwa jinsi Benki ya CRDB inavyojitolea kudumisha uendelevu na tunaona kushirikiana na benki hiyo kuingia DRC kama fursa nzuri ya kukuza ushirikishwaji wa kifedha na kuchangia uzalishaji wa ajira katika nchi ambayo watu wengi hawana benki.
Naye Makamu wa Rais wa IFU, Morten Elkjær alibainisha kuwa kuendelea kuwekeza kwa Benki ya CRDB katika programu endelevu za kilimo cha kukabiliana na hali ya hewa na nishati safi kumeifanya kuwa mshirika wa kimkakati na kiongozi wa fikra.
"Tunazingatia hasa uwekezaji ambao unasaidia mabadiliko ya kijani kibichi na kuchangia katika kupunguza umaskini na kupunguza ukosefu wa usawa," alisema Elkjær.
Benki ya CRDB ni benki ya kwanza ya Kitanzania kujitosa nchini DRC, ambayo inachukuliwa kuwa mshirika mkubwa wa kibiashara wa nchi hiyo.
Mwaka 2019 Tanzania na DRC zilitia wino makubaliano ya pande mbili ya ujenzi wa Reli ya Standard Gauge inayounganisha nchi hizo mbili kupitia Burundi.
No comments:
Post a Comment