Kauli ya Wakili Kambole imekuja siku chache wakati wadau wa habari wakiendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha kuwa vifungu vya sheria vinavyoonekana kukandamiza tasnia ya habari vinafanyiwa marekebisho.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo juu ya Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 na ile ya Makosa ya Mtandaoni ya 2015, Kambole amesema makosa yote yanayofanywa na waandishi wa habari yanapaswa kuwa ni makosa ya kimaadili na isiwe kosa la jinai linalopelekea vifungo.
Ameeleza kuwa Sheria hiyo inakikuka Mkataba wa Kimataifa na ule wa Afrika Mashariki katika Ibara ya 7(b) ambapo wadau wa habari ikiwemo Baraza la Habari Tanzania (MCT) na wengine wawili walifungua kesi katika Mahakama ya Afrika Mashariki namba 2, 2017.
“Katika kesi hiyo Mahakama ya Afrika Mashariki ilitoa hukumu iliyoeleza kuwa sheria hiyo inakiuka haki za msingi na kuvitaja baadhi ya vifungu.
“Baadhi ya vifungu vya 7, 21, 35, 36, 37, 38, 39, 40, 50, 51, 52, 53, 58 na 59 vya Sheria ya Huduma za Habari inakiuka Mkataba wa Afrika Mashariki na ili kuepuka vifungo lazima waandishi wa habari waandike habari zinazoipendelea serikali,”amesema Kambole.
Kambole ameongeza kuwa kupitia sheria hiyo vyombo vya habari haviko huru katika kutekeleza majukumu hivyo kupelekea kutokuwepo kwa habari za kiuchunguzi ambazo husaidia maendeleo ya Taifa ikiwemo masuala ya rushwa na mengine.
Hata hivyo Kambole amebainisha kuwa sheria hiyo pia inatoa mamlaka ya mwandishi wa habari kunyang’anywa utambulisho wake au kibali cha kufanya kazi za uandishi hivyo kutoa hofu kwa wahusika kutofanya kazi yao ili kulisaidia taifa.
Awali Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Nevile Meena amesema Bodi ya Ithibati ya Habari ikiwa itaundwa na Serikali basi itakosa uhuru wa kufanya uamuzi pale malalamiko yatakapoihusu yenyewe (serikali).
Meena ambaye ni Katibu Mstaafu wa TEF amesema, ili kukwepa hilo na kutenda haki kwa vyombo vyote vya habari nchini, hakuna budi kwa Bodi ya Ithibati ya Habari kuundwa na kusimamiwa na wanataaluma haswa wanahabari.
No comments:
Post a Comment