Na Asha Mwakyonde
MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), imesema kuwa ili mtu apate kipimo cha Vinasaba (DNA), lazima aonane na Afisa Ustawi wa Jamii katika eneo husika au Wakili aliyeandikishwa ndiye atakayepeleka ombi la kipimo hicho kwa Mkemia wa Serikali.
Vinasaba ni chembe chembe za uhusiano wa urithi zinazotokana na kizazi kimoja kwenda kingine.
Akizungumza Julai 7,2022 katika Maonyesho ya 46 ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu Saba Saba yanayaofanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Mkemia wa Serikali Dk. Fidelice Mafumiko amesema huduma ya elimu kuhusiana na kipimo cha Vinasaba inapatikana katika banda la mamlaka hiyo lililopo katika jengo la Jakaya Kikwete kwa maana kujua utaratibu ukoje.
Mkemia huyo amesema kuna Mamlaka ambazo zimeidhinishwa kisheria na mteja anataka kupima kwa ajili ya nini.
"Mtu akija katika banda hili ili apate elimu tunaangalia suala lake ni suala la jinai au ni suala la kijamii kwa mfano anataka kufahamu uhalali wa mtoto kwa mzazi au uhalali wa mzazi kwa mtoto, tuna mwambia ili apate kipimo hiki lazima aonane na Afisa Ustawi wa Jamii katika eneo lake au Wakili aliyeandikishwa," amesema.
Dk. Mafumiko amefafanua kuwa afisa huyo ndiye atakayepeleka shida ya mteja wake kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kupata kipimo cha Vinasaba.
Akizungumzia gharama Mkemia huyo amesema kwa kila mtu atakayechukuliwa sampuli ni shilingi laki 100,000 hivyo ikiwa ni baba,mama na mtoto itakuwa laki 300,000.
" Kuhusiana na masuala ya jinai kama ubakaji inategemea ni watu wangapi wanaochukuliwa sampuli waliohusika na tukio kikubwa gharama ni laki moja kwa kila mtu," ameeleza.
Amefafanua kwamba gharama hiyo ni ya chini kabisa kwa kuwa mahitaji ya dawa zinazotumika, muda na utaalamu gharama yake ni laki 700,000 hadi 800,000.
Dk. Mafumiko ameeleza kuwa Serikali imewekeza katika Mamlaka hiyo vifaa na utaalamu ndio maana ni 100,000 kupima Vinasaba na gharama hiyo imedumu kwa miaka mingi.
Amewataka wahitaji wa kipimo hicho kupata maelezo Sahihi ya mahitaji yao na wanaweza kuyapata katika banda la mamlaka hiyo.
No comments:
Post a Comment