HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 18, 2022

RAIS SAMIA AMLILIA MPIGANIA UHURU AFRIKA KUSINI

Marehemu Yasmin ‘Jessie’ Duarte enzi za uhai wake.

 

 Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa Chama Cha African National Congress (ANC) Gwede Mantashe na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, kutokana na kifo cha aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa ANC, Yasmin ‘Jessie’ Duarte aliyefariki dunia Julai 17 mwaka huu.


Amesema marehemu Jessie alikuwa mmoja wa viongozi imara wa ANC, tangu enzi za mapambano ya kupinga ubaguzi wa rangi nchini humo.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, ilisema Rais Samia amesema atamkumbuka kiongozi huyo kwa namna alivyokuwa anasimamia utu, kwa ajili ya jamii yenye usawa bila kujali jinsia na rangi.

“Nimepokea taarifa za msiba huu kwa masikitiko makubwa. Salamu za rambirambi katika wakati huu mgumu ziwafikie familia yake, ndugu, jamaa na marafiki na wote walioguswa na msiba huu. 

“Tuko pamoja na makomredi wote wa ANC, Afrika Kusini kwa ujumla, Afrika na kwingine kote duniani ambao mbali ya kuguswa na maisha ya kikazi ya Komredi Jessie, pia walishirikiana naye kwa namna moja au nyingine kutekeleza wajibu wa kizalendo, kupigania na kulinda uhuru wa Mwafrika na nchi za Afrika katika nyanja mbalimbali,”ailisema.

Aidha, tarifa hiyo ilisema Rais Samia, alisema hatua ya Jessie kuaminiwa kuwa msaidizi maalumu wa Hayati Nelson Mandela, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha ANC tangu mwaka 2002 na kuwa Naibu Katibu Mkuu wa ANC tangu mwaka 2012, inadhihirisha uwezo wake wa kiuongozi, uimara na umuhimu wake kwa chama hicho. 

Rais Samia alisema marehemu Jessie, alikuwa sehemu ya mafanikio kwa chama hicho tangu zama za kupigania ukombozi, kwa ajili ya jamii yenye ustawi wa haki, usawa na maendeleo ya watu wa Afrika Kusini na Afrika kwa ujumla.


No comments:

Post a Comment

Pages