Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akichangia jambo kwenye Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika jijini Lusaka, Zambia.
Waziri
Mulamula ametoa wito huo alipokuwa akichangia ajenda iliyohusu masula
ya nafasi za uanachama katika Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa
Afrika kwenye Mkutano wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika
uliofanyika jijini Lusaka Zambia tarehe15 Julai 2022.
Akitoa
mchango wake kwa lugha ya Kiswahili Waziri Mulamula alieleza kuwa
Tanzania inaunga mkono juhudi zinazofanywa na AU kwa lengo la kuimarisha
utendaji wa Baraza la Umoja na Usalama la Umoja wa Afrika ikiwemo
kuendelea kuwa na idadi ya wanachama waliopo katika baraza hilo.
“Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ni muumini mkubwa wa usawa wa uwakilishi wa
kanda na nchini wanachama ndani ya Umoja wa Afrika na Taasisi nyingine
za kimataifa. Hii ni kutokana na imani yetu kuwa endapo usawa
utazingatiwa tutaendelea kudumisha umoja na mshikamano wetu ambao kwa
muda mrefu umeendelea kuwa nguzo ya amani na usalama katika bara letu” Alieleza Waziri Mulamula.
Sambamba
na hilo katika Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri miongoni mwa ajenda
zilizojadiliwa ilikuwa ni kupitisha bajeti ya Umoja wa Afrika kwa mwaka
2023. Kitu muhimu katika mkutano huu ni kuwa bajeti hiyo imeweka kifungu
kwa ajili ya utekelezaji wa maamuzi ya Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi
na Serikali wa Umoja wa Afrika yaliyopitsha Kiswahili kuwa Lugha ya Kazi
ya Umoja wa Afrika.
Akizungumzia
suala hilo Waziri Mulamula ameeleza kuwa amefarijika kuona kipengele
maalumu cha kutekeleza maamuzi ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kazi
ya Umoja wa Afrika inafanyiwa kazi kwa vitendo. Aliongeza kusema hatua
hiyo itaharakisha utekelezaji wa maamuzi hayo kwa kuwa itarahishisha
utendaji wa shughuli mbalimbali muhimu kama vile kugharamia zoezi la
kutafsiri nyaraka mbalimbali, kulipa au kuajili wakalimani na kuwajengea
uwezo wa lugha hiyo wataalamu wa ngazi mbalimbali katika Kamisheni ya
Umoja wa Afrika na Taasisi nyingine za umoja huo.
Aidha
katika mkutano huo wa 41 wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika kwa
mara ya kwanza wameanda baadhi ya taarifa zinazotokana na mkutano huo
kwa lugha ya Kiswahili.
Vilevile
Waziri Mulamula kwenye Mkutano huo alichangia mjadala wa kupitisha
bajeti ya Umoja wa Afrika kwa mwaka 2023 ambapo kwa niaba ya Tanzania
ameunga mkono mapendekezo ya bajeti ya umoja huo. Pia alitumia nafasi
hiyo kutoa wito kwa Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Taasisi zake
kuendelea kuchukua hatua za kupunguza matumizi ili kuendana na uhalisia
wa hali ya uchumi wa nchi zetu za Afrika katika nyakati hizi.
“Tunatoa
wito kwa Kamisheni na Taasisi nyingine za Umoja wa Afrika kuweka
mipango mizuri ya miradi na shughuli zake ili kuendana na uwezo wa
kutekeleza miradi hiyo na kuweka kipaumbele kwa miradi yenye tija kwa
wananchi wa Bara la Afrika” Alisema Waziri Mulamula.
Mkutano
wa 41 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa Afrika umeongozwa na mwenyekiti
wake Mhe. AissataTall Sall ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa
Senegal
No comments:
Post a Comment