Mkurugenzi wa Kozi za Shahada na zisizokua za Shahada wa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (RUCU) Dk. Wille Migodela (wa kwanza kutoka kushoto) akitoa maelekezo kwa baadhi ya Wanafunzi waliotembelea banda lao la Maonesho ya TCU.
Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (RUCU) kimewakaribisha wazazi na walezi kuwaleta watoto wao katika Banda lao la Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ili wafanye uchaguzi sahihi wa kozi wanazotaka kuzisoma huku kikibainisha kujikita kutoa elimu ya utafiti bunifu kwa wanafunzi ili kuwawezesha kukabiliana na changamoto zinazoikabili jamii pamoja na kuondokana na dhana ya kuajiriwa badala yake waweze kujiajiri baada ya kuhitimu masomo yao.
Miongoni mwa tafiti bunifu zinazofanywa chuoni hapo ni Utafiti wa changamoto za kimazingira ikiwemo wa kukabiliana na Mbu wanaoambukiza Ugonjwa wa Malaria, ya ngozi (Fangasi) na Kikohozi, ambapo wanafunzi wanafanya tafiti kupitia mimea ya asili na kutengeneza dawa ambazo zinasaidia kukabiliana na magonjwa hayo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kozi za Shahada na zisizo za Shahada wa RUCU, Dkt. Wille Migodela wakati akizungumza na Wanahabari kwenye Maonesho ya 17 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Nchini ( TCU) yanayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.
Amebainisha kuwa chuo hicho kinatoa programu za kozi mbalimbali ila elimu ya utafiti wa ubunifu imekua ikipewa kipaumbele ili kumsaidia mwanafunzi anaehitimu kuacha kutegemea kuajiriwa na badala yake kumjenga kujiajiri.
Amesisitiza kuwa wanafunzi wanaosoma chuo hicho wamefanikiwa kubuni kifaa kinachopima uzito wa mizigo inayobebwa na magari ambapo kifaa hicho kinafungwa kwenye gari na kwamba gari hiyo haitapita kwenye mzani kwa ajili ya kupimwa, badala yake kifaa hicho kitaonyesha ukomo wa uzito kamili unaohotajika kubebwa na gari hilo.
"Magari yanatumia muda mrefu kukaa kwenye foleni ya mizani kupima uzito wa mzigo, RUCU tumekuja na suluhisho la kubuni kifaa Cha kisayansi kitakachoonesha ukomo wa uzito wa mzigo unaotakiwa kupakiwa" amesema Dkt. Migodela
Pia amesema kuwa mwaka huu wa masomo 2022/ 2023 wanatarajia kudahili wanafunzi ngazi ya Cheti na Diploma ni 700 huku shahada wakitarajia kudahili wanafunzi 700.
Miongoni mwa kozi zinazotolewa na chuo hicho Ngazi ya Cheti, Astashahada na Shahada na Shahada ya Uzamivu ni Utawala wa Biashara, Sheria, Sayansi ya Kompyuta, Teklonojia ya habari, Sayansi ya Afya ya Mazingira na Ualimu.
No comments:
Post a Comment