Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Shirika
la Reli Tanzania (TRC) limefanya hafla fupi ya utiaji saini Mkataba wa
Ukarabati wa Behewa 20 za mizigo wakishirikiana na Taasisi ya Ushoroba
wa Kati (CCTTFA).
Tukio hilo limefanyika jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Mikutano wa Shirika hilo.
Akizungumza na wanahabari baada ya utiaji saini mkataba huo, Mwenyekiti wa Bodi kutoka TRC Profesa John Kondoro ameipongeza Taasisi ya Ushoroba wa Kati kwa kuongeza nguvu kwa TRC katika ukarabati wa behewa hizo kwa ajili ya reli ya zamani ambazo zitagharimu kiasi cha fedha za Tanzania Bilioni moja milioni ishirini na tatu, thelathini na moja elfu na mia tano arobaini na tano (1,023,031,545.60).
Profesa Kondoro amebainisha kuwa njia ya reli ya zamani imedumu zaidi ya miaka mia moja hivyo inahitaji ukarabati wa mara kwa mara pamoja na ukarabati wa vichwa na behewa.
“Jinsi ambavyo muda unakwenda mahitaji yanaongezeka kwa maana kwamba uzalishaji umekua mkubwa na watu wangependa wapate huduma” alisema Profesa Kondoro.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TRC Masanja Kadogosa ameeleza kuwa ukarabati huo wa behewa 20 za mizigo utachukua takribani miezi 24.
“CCTTFA wameonyesha nia ya kushirikiana na TRC katika kufanya kazi ya ukarabati wa behewa hizo hivyo tumewapa nafasi hiyo” amesema Kadogosa.
Kadogosa amesisitiza kuwa nia na madhumuni ya ukarabati huo ni kuipa uwezo TRC katika usafirishaji wa mizigo kwa kutumia reli ya zamani ili kuendeleza ufanisi wa kazi za kusafirisha behewa za mizigo.
Hata hivyo Ndugu Kadogosa ameeleza kuwa TRC inafanya biashara ya usafirishaji wa mizigo na nchi jirani ikiwemo nchi ya Uganda, Rwanda, Burundi na Congo hivyo kupitia ukarabati huo itasaidia kuongeza uwezo wa kuwa na vitendea kazi vyakutosha.
Aidha Kadogosa ameishukuru serikakali kwa kutoa fedha kwaajili ya kutekeleza mradi wa ukarabati wa behewa 200 za mizigo sambamba na hilo TRC ilianza mkakati wa kushirikiana na wadau katika ukarabati wa behewa za mizigo ambapo TRC pamoja na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani - WFP yatiliana saini makubaliano ya ukarabati wa mabehewa 40 ya mizigo mwezi Machi, 2019.
Naye Katibu Mtendaji Mkuu wa Central Corridor Wakili Flory Okanju amesema kuwa lengo ni kuweza kurahisisha biashara katika nchi jirani ikiwemo Tanzania, Burundi, Congo, Uganda pamoja na Rwanda kwa kutumia Reli.
“Sekta ya reli inasaidia sana kwa kuwa na bei nafuu na kulinda mazingira ya nchi na ushoroba wa kati pamoja na kulinda barabara” alisema Adv. Okanju.
Pia Shirika la Reli limetoa fursa kwa wadau kushirikiana na TRC katika kuboresha usafiri wa reli nchini ikiwemo ukarabati na ujenzi wa miundombinu pamoja ukarabati wa behewa ili kuongeza ufanisi wa sekta ya reli nchini.
No comments:
Post a Comment