Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua Daraja la mawe lenye urefu wa mita 30 na upana wa mita saba lililojengwa katika Kijiji cha Lukomo barabara ya Iguguno-Kikhonda-Kinampundu wilayani Mkalama wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya leo wilayani humo mkoani Singida leo.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Singida, Martha Gwau, akizungumza kwenye ukaguzi huo. |
Na Dotto Mwaibale, Mkalama, Singida
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amekagua daraja la mawe lililojengwa na Wakala
wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Singida na kuokoa
Sh.448 milioni, daraja lililojengwa katika Kijiji cha Lukomo wilayani
Mkalama kwa kutumia teknolojia mpya ya mawe.
Akizungumza kabla ya Waziri Mkuu hajalikagua daraja hilo Meneja wa TARURA
Mkoa wa Singida, Tembo David, alisema kwa kutumia teknolojia mpya ya kulijenga
kwa mawe limegharimu Sh.102 milioni.
" Daraja hili kama tungelijenga kwa njia ya kawaida lingeigharimu
Serikali Sh.550 milioni lakini kwa kutumia teknolojia hii ambayo ni nafuu
sana inatumika nchini Hispania na hapa
nchini madaraja kama hayo yamejengwa Mikoa ya Kigoma na Mbeya," alisema.
David alisema ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 30 na upana wa mita
7 ulianza Disemba 18, 2021 na limekamilika Julai 18, 2022.
Meneja huyo aliishukru serikali kwa kuongeza bajeti ya ujenzi wa barabara
katika Mkoa wa Singida kutoka Sh.6 bilioni hadi kufikia Sh.23.4 bilioni.
Waziri Mkuu, Majaliwa, aliwapongeza Wahandisi wa Mkoa wa Singida kwa
ubunifu huo mpya wa ujenzi wa daraja hilo na kutaka teknolojia hiyo isambae
katika mikoa yote nchini.
"Kupitia vikao vyenu vya TANROAD na TARURA hii taaluma muifikishe kwa
mainjinia ili kila injinia kwenye mkoa wake atafute fursa na bahati nzuri mawe
yamejaa kwenye maeneo yetu," alisema.
Majaliwa alisema serikali imekuwa ikigharamia fedha nyingi kujenga madaraja
kwa gharama kubwa wakati kumbe kuna Watanzania wabunifu wenye taaluma zao
wanaweza kujenga madaraja kwa gharama nafuu.
"Daraja hili hapa miaka yote tulishindwa kulijenga sababu ya gharama
na ilikuwa lazima tupate zaidi ya shilingi milioni 500 kumbe mainjinia wetu na
usomi wao wana uwezo wa kujenga daraja la kudumu kwa gharama nafuu,"
alisema.
Aidha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
baada ya kukagua daraja hilo alipata
fursa ya kuzindua Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama lililokamilika
kwa asilimia 100 ambalo limejengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa
gharama ya Sh. 1.33 Bilioni bila ya VAT.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk. Festo Dugange, alisema serikali
imekubaliana na wahandisi wa TARURA kuendelea kuwa wabunifu na kwamba Wilaya ya
Mkalama imeongezewa bajeti ya ujenzi wa barabara kutoka Sh.600 milioni hadi kufikia
Sh.2.2 bilioni.
No comments:
Post a Comment