Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona (wa pili kulia) akimuelekeza jambo Mwanamfalme wa Falme ya Babina Noko Ba Mampuru ya Limpopo Afrika Kusini, Spumendo Mokgabudi nje ya ofisi za Bodi ya Mkonge jijini Tanga.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona (wa pili kulia) akishikana mikono na Mwanamfalme wa Falme ya Babina Noko Ba Mampuru ya Limpopo Afrika Kusini, Spumendo Mokgabudi kama ishara ya kumkaribisha alipomtembelea ofisini kwake jijini Tanga. Kulia ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Zao la Mkonge, Olivo Mtung'e na kushoto ni Mkurugenzi wa Kampuni ya D.D. Ruhinda, Deo Ruhinda.
Na Mwandishi Wetu, Tanga
BODI ya Mkonge Tanzania (TSB), imesema iko tayari kushirikiana na Falme ya Babina Noko Ba Mampuru iliyopo katika Jimbo la Limpopo nchini Afrika Kusini kuendeleza zao la mkonge katika mambo mbalimbali ikiwamo kutoa wataalamu wake na kubadilishana uzoefu baina ya nchi hizo mbili.
Kaimu Mkurugenzi wa TSB, Saddy Kambona amesema hayo jana, wakati akizungumza na Mwana wa Mfalme wa Falme ya Babina Noko Ba Mampuru, Spumendo Mokgabudi aliyemtembelea ofisini kwake jijini Tanga jana.
Mwana wa Mfalme Mokgabudi, yuko hapa nchini kwa ziara binafsi kwa ajili ya kufanya utafiti na kujifunza mambo mbalimbali kuhusu kilimo cha mkonge akiwa na mpango wa kuanzisha kilimo hicho kwenye falme yake ambapo akiwa Tanga amekutana na Menejimenti ya Bodi ya Mkonge na uongozi wa Kampuni ya D.D. Ruhinda.
Katika mzungumzo yao, Mokgabudi amemuomba Kambona kumsaidia mambo matatu ikiwamo kuiomba Bodi ya Mkonge imsaidie upatikanaji wa mbegu za mkonge kwa ajili ya falme yake.
“Tumepata ugeni wa Mwana wa Mfalme kutoka Afrika Kusini, tumezungumza mengi lakini kikubwa ni kuhusu suala zima la zao la mkonge na miongoni mwa mambo aliyoomba mbali na upatikaji wa mbegu ni kubadilishana wataalamu ambao watakuja nchini na wa hapa nchini kwenda kule ili kujifunza mambo mbalimbali kuhusu mkonge na mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo na jambo la tatu ni kusaidia utaalamu na miongozo mbalimbali itakayowezesha Falme ya Babina Noko Ba Mampuru kuanzisha bodi yake ya mkonge.
“Tuko tayari kushirikiana na kampuni hiyo ya Babina Noko Mampuru kwa kutoa wataalamu wa zao la mkonge kwa ajili ya kwenda kutoa mafunzo kwa wataalamu wengine wa falme hiyo nchini Afrika Kusini. Lakini pia tumekubaliana kubadilishana uzoefu kwa kubadilishana wataalamu wetu ambao watakuwa wanakuja huku na wa kwetu wanakwenda kule.
“Sisi kama Bodi ya Mkonge tumemuahidi ushirikiano lakini si tu na falme hiyo, bali Afrika Kusini kwa ujumla ambapo tutafikisha maombi hayo kwa wizara mama (Wizara ya Kilimo) ili taratibu nyingine ziweze kuendelea katika kusaidia falme hiyo kuendeleza zao la mkonge,” alisema Kambona.
Pamoja na mambo mengine, amesema ardhi na hali ya hewa ya nchi hiyo inaruhusu kilimo cha mkonge hivyo hiyo ni fursa ambayo wanatarajia itawanufaisha wengi nchini humo.
Kwa upande wake Prince Mokgabudi, alisema atarudi wakati mwingine ili kujifunza zaidi kwa kuzunguka maeneo mengi zaidi kwani hii ni ziara yake binafsi nchini na katika mikakati ya kuanzisha kilimo cha mkonge nchini Afrika Kusini tayari wanazo hekta milioni tatu zilizotengwa kwa ajili hiyo.
“Nimekuja kujifunza kwa jicho la awali, nimejionea na nimejifunza mambo mbalimbali na nimevutiwa kuanzisha kilimo cha mkonge nchini kwetu kwani ya ardhi inaruhusu na hali ya hewa pia ni kama ya hapa.
“Licha ya kuanzisha kilimo hicho cha mkonge nchini kwetu lakini pia tuna mpango wa kuanzisha bodi yetu ya mkonge itakayokuwa na jukumu la kusimamia kikamilifu zao la mkonge na mambo mbalimbali yanayohusu zao hilo.
“Kwa leo tumekuja kufanya mazungumzo kwa ajili ya kuanzisha ushirikaino kati ya Tanzania na Afrika Kusini kupitia Bodi ya Mkonge Tanzania, mipango yetu ni tukishaanzisha bodi yetu na sisi itakuwa ni chombo chenye kusimamia udhibiti wa zao la mkonge, uzalishaji na masoko,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya D.D Ruhinda Ltd. Deo Ruhinda alisema ushirikiano huo utaleta tija kwani kutakuwa na uhakika baina ya nchi hizo mbili.
“Ni uwekezaji mkubwa na mzuri ambao serikali ikiridhia hata sisi tutanufaika kwani chapa yetu itakuwa inatumika kama alama ya biashara. Ni mradi mkubwa ambao utakuwa na mambo mengi kama kupeleka mbegu na masoko lakini hatuwezi kuingia nao moja kwa moja bila serikali kutia mkono humo.
“Kwetu sisi watapata uzoefu kupitia mashamba yetu, kampuni na viwanda. Kwa upande wao sasa sera ya serikali ya kule waangalie watengeneze vipi sera zao kwa sababu kule kwao mkonge wameweka chini ya wizara ya madini kuna mambo mengi watahitaji kutoka upande wa serikali na binafsi,” alisema.
No comments:
Post a Comment