Mwenyekiti
wa Kamati ya Ripoti ya Utafiti wa Watalii ambaye ni Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma S. Mkomi akisoma ripoti ya Matokeo
ya Utafiti wa Watalii Walioondoka nchini mwaka 2021 mara baada ya
uzinduzi wa ripoti hiyo iliyotolewa leo Ijumaa Septemba 30, 2022 Jijini
Arusha.
Na Mwandishi Wetu
Idadi ya mapato yatokanayo na utalii imeongezeka kutoka
Dola za Kimarekani milioni 714.59 kwa mwaka 2020 hadi kufikia Dola za
Kimarekani milioni 1,310.34 kwa mwaka 2021
Taarifa
hiyo imetolewa leo Ijumaa Septemba 30, 2022 Jijini Arusha na
Mwenyekiti wa Kamati ya Ripoti ya Utafiti wa Watalii ambaye ni Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma S. Mkomi wakati wa
uzinduzi wa ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Watalii Walioondoka nchini
mwaka 2021.
Naibu Katibu
Mkuu Mkomi amesema taarifa ya utafiti huo inaonesha kuwa Tanzania
inazidi kufanya vizuri katika sekta ya utalii huku mapato yatokanayo na
utalii yakiongezeka mwaka hadi mwaka.
Amesema
mwaka mmoja baada ya mlipuko wa janga la UVIKO-19, idadi ya watalii
iliongezeka kutoka watalii 620,867 mwaka 2020 hadi kufikia watalii
922,692 mwaka 2021 ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 48.6
Amezitaja
sababu zilizochangia ongezeko la watalii hapa nchini mara baada ya
mlipuko wa Janga la UVIKO 19 kuwa ni jitihada zinazofanywa na Serikali
pamoja na Sekta binafsi katika kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje
ya nchi
Mkomi amesema,
matokeo ya utafiti yanaonesha idadi kubwa ya watalii walikuja hapa
nchini kwa ajili ya kutembelea hifadhi za wanyamapori na fukwe.
Utafiti
huo umefanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na
Benki Kuu Tanzania (BOT), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Idara ya
Uhamiaji, Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Shirikisho la wawekezaji
katika Sekta ya Utalii Zanzibar ( ZATI)
Mkomi
amesema takwinu za utafiti huo, zimepatikana kutokana na utafiti
uliofanywa katika vituo vikubwa nane vya watalii, ikiwemo viwanja vya
ndege vya kimataifa pamoja na maeneo ya njia za kuingilia na kutokea
watalii.
Matokeo ya
utafiti huo yameonesha kuwa idadi kubwa ya watalii wametokea nchi ya
Ufaransa ikifuatiwa na Marekani, Kenya pamoja na Zambia
Katika
hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu Mkomi amesema matokeo ya utafiti huo
yameonesha kuwa wastani wa matumizi ya mtalii kwa siku hapa nchini
yaliongezeka kutoka dola za Kimarekani 152 mwaka 2020 hadi kufikia dola
za Kimarekani 199 mwaka 2021
Naye,
Kaimu Mkurugenzi wa Utalii Wizara ya Maliasili na Utalii, Richie
Wandwi amesema kwa sasa Wizara ya Maliasili na Utalii imejidhatiti
kuwekeza nguvu katika utalii wa fukwe kwa vile ni aina ya utalii ambao
unaonekana kupendwa na watalii wengi wanaoingia nchini.
Ameongeza
kuwa, Wizara itaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali ambazo
baadhi ya watalii wamekutana nazo ili kuhakikisha idadi ya watalii
inazidi kuongezeka na vivutio vilivyopo hapa nchini vinatangazwa kwa
kasi zaidi katika Jumuia za Kimataifa.
Utalii
ni miongoni mwa sekta muhimu katika uchumi wa dunia ambapo idadi ya
watalii duniani iliongezeka kwa takribani asilimia tano na kuchangia
asilimia 6.8 ya mauzo ya nje, na kuzalisha ajira milioni 333.
No comments:
Post a Comment