TANI zaidi 1593 za zao la mbaazi zimeweza kununuliwa katika mnada wa kwanza wa mbaazi wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Meneja wa Ghala Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU) Sarah Chorwa amesema ununuzi huo umefanyika kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kwenye vyama vya ushirika vya msingi.
Hata hivyo amesema mnada wa pili unatarajia kufanyika Alhamis wiki hii ambapo hadi sasa tayari wana tani 135 na upokeaji wa mbaazi bado unaendelea.
“tunatarajia hadi mwisho wa msimu huu kufikisha tani zaidi ya 5,000 za mbaazi’’alisema Chorwa.
Amesema katika msimu huu kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani waliweza kununua zao la ufuta zaidi ya tani 2500.
Amesema mfumo wa stakabadhi ghalani ni mzuri na wakulima wengi wameukubali na kwamba unawarahisishia wanunuzi kupata mzigo kwa pamoja.
Amesema mfumo huo unawanufaisha watu mbalimbali wakiwemo wasafirishaji,makuli na akinamama lishe na kwamba serikali inapata mapato yake kwa urahisi.
Kwa upande Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumzia Mfumo huo amesema mfumo wa stakabadhi ndiyo mkombozi wa wakulima kwa sababu unatoa soko la uhakika kwa wakulima.
Hata hivyo Amesema kuna siasa zinapigwa chini chini kuonekana kama mfumo huo haufai .
Amesema serikali ya Mkoa imefanya mawasiliano na Wizara ya kilimo kupata kibali cha kuuza mbaazi kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo tayari mnada wa kwanza umefanyika wilayani Tunduru na wananchi wengi wamejitokeza na wanafaidika.
Ametahadharisha kuwa wafanyabiashara ambao hawawatakii mema wakulima ndiyo wanaopambana kuhakikisha Mfumo huo unakufa ili wao waweze kufaidika.
Amesisitiza kuwa wafanya biashara hao walikuwa wanawaibia wakulima kupitia pembejeo za kilimo ambapo hivi sasa Mheshimiwa Rais ametoa ruzuku ya mbolea kutoka shilingi 130,000 kwa mfuko ambayo imeshuka kati ya shilingi 70,000 hadi 50,000 kwa mfuko kutegemea na aina ya mbolea.
“Nawashauri na kuwasisitiza kuwa Mfumo wa stakabadhi ghalani una faida kubwa zaidi kuliko uuzaji holela “,alisema RC Thomas.
Nao wakulima katika wilaya za Tunduru,Songea na Namtumbo wametoa rai kwa serikali kuhakikisha mfumo unakuwa endelevu kutokana na faida nyingi wanazopata wakulima.
Ahmed Salehe Mkulima wa Ligunga Tunduru Amesema mfumo wa stakabadhi ghalani umeongeza Usalama wa fedha za mkulima na umechangia kutoa ajira katika makundi mbalimbali.
Amesema Mfumo huo unatoa bei sawa kwa wakulima wote ambapo ametolea mfano kwenye mnada wa zao la mbaazi mkulima amenunua kwa kilo shilingi 800.
Sophia Mambo mkulima wa Mbesa Tunduru amesema kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani wakulima wanapata bei kubwa ya mazao wakati kwenye Mfumo holela wakulima wananyonywa kwa kuuza mazao bei ya chini.
Basilius Komba Mkulima wa Ndongosi Songea amesema wakulima walikuwa wanateseka kwenye Mfumo holela ambapo Mfumo wa stakabadhi ghalani umekuwa rafiki kwa mkulima na wanapata faida kubwa.
Mazao ambayo yanauzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani mkoani Ruvuma ni ufuta,soya,mbaazi,korosho na kahawa.
Imeandikwa na Albano Midelo, Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ruvuma
No comments:
Post a Comment