HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 19, 2023

Kusini waongoza kwa uvamizi wa Ardhi- SMZ

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Rahma Kassim Ali (Kati), Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Mzee Ali Haji ( kusho) na Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Rajab Mkasaba wakizungumza masheha wa Wilaya hiyo kuhusu uvamizi wa ardhi ya akiba.


 

Na Mwandishi Wetu

 

Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar imesema kumekua na uvamizi pamoja na uuzaji holela wa maeneo ya ardhi ya akiba kitendo ambacho kinachangia ongezeko la migogoro ya ardhi Zanzibar.

 

Kauli hiyo imetolewa jana na waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar Rahma Kassim Ali alipokutana na Masheha wa Wilaya ya Kusini Unguja, kikao maalum kilichofanyika ofisi za Mkuu wa Wilaya hiyo alisema   kumekua na uvamizi na uuzaji holela wa maeneo ya ardhi ya akiba yaliyotengwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

 

Waziri Rahma alisema Wizara yake itahakikisha inaweka mikakati imara ya udhibiti wa uuzaji ardhi kiholela hasa katika maeneo ya ardhi ya akiba yaliyotengwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

 

Aidha alieleza kwamba Wilaya ya Kusini Unguja inaongoza kwa uvamizi na uuzaji wa  ardhi kiholela hasa katika maeneo ya fukwe za bahari yiliyopo wazi  hivyo kutokana uwezo wa wizara yake kupewa dhamana ya usimamizi wa ardhi kwa mujibu wa tangazo la kisheria Nam 137 ya Mwaka 2020 itahakikisha inayadhibiti maeneo hayo.

 

“ Wilaya ya kusini Unguja  inaongoza kwa uvamizi na uuzaji wa maeneo kiholela hasa maeneo ya fukwe na yaliyo wazi  hivyo kwa vile Wizara yangu ndio iliyopewa dhamana ya usimamizi wa ardhi kwa mujibu wa sheria nitahakikisha ninayadhibiti maeneo hayo na atakaebainikia kwenda kinyume hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake” Alisema waziri huyo.

 

Hivyo  Waziri huyo amewataka masheha hao kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika usimamizi wa masuala ya ardhi pamoja na kufanya kazi zao ipasavyo kwa kutojihusiha na vitendo vya uuzaji wa ardhi bila kufuata sheria zilizowekwa.

 

Naye Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Mzee Ali Haji alitoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya ardhi kwa wageni ambapo alisema kwa mujibu wa Sheria ya ardhi Nam.12 ya mwaka 1992 imekataza kuuziwa ardhi mgeni yeyote bali atatakiwa kukodishwa kwa ajili ya uwekezaji na sio vyenginevyo.

 

Kwa upande Mkurugenzi Mipango Miji na Vijiji Kutoka Kamisheni ya Ardhi Muchi Juma Ameir alisema tayari Kamisheni ya Ardhi  imeyaainisha  maeneo yote yenye ardhi ya akiba yaliyoko katika Mkoa wa Kusini Unguja yakiwemo Paje, Muungoni,na Muyuni kwa lengo la kuyapanga na kuyapima kwa kuyawekea alama na  kuyadhibiti ili yasiweze kuvamiwa kwa uuzaji wa viwanja kiholea.

 

Kwa upande wa mashe Shehia ya paje Mohammed Rajabu Makame alisema kuwa  kwa kiasi kikubwa wanasheria ndio wanaohusika na masuala ya ukiukwaji wa sheria kwa kufanya vitendo hivyo na hata wao kuwakosesha ufanisi mzuri wa kiutendaji hasa katika kazi zao za usheha.

 

Mapema Mkuu wa Wilaya ya Kusini Rajab Mkasaba alimkaribisha waziri huyo na kuwataka masheha kuwa mabalozi wazuri katika kutoa elimu kwa jamii juu ya umiliki wa ardhi katika shehiya zao.

 

Kikao hicho kimefanyika kwa lengo la kujadili na kuweka mipango mikakati  ya usimamizi madhubutu ambao utasaidia kuondoa changamoto ya uuzaji wa ardhi kiholela  pamoja na kupunguza migogoro ya ardhi nchini.


No comments:

Post a Comment

Pages