HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 01, 2023

MARUFUKU WANANCHI WA VIJIJJ 11 KUFANYA SHUGHULI ZA KIBINADAMU MAENEO YA HIFADHI LINDI-DKT MABULA


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mtepera wilayani Kilwa mkoa wa Lindi wakati Kamati ya Mawaziri wa Wizara ya Kisekta walipotembelea kijiji hicho Desemba 29, 2022. Wa pili kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Lindi Zainab Telack.

 

 

 Na Munir Shemweta, WANMM LINDI

 

Waziri wa ardhi Nyumba na maendeleo ya makazi Mhe Dkt Angeline Mabula amepiga marufuku ufanyaji shughuli za kibinadamu katika maeneo ya hifadhi ya msitu wa Nyengedi na Pori la Akiba la Selous mkoani Lindi.

 

Dkt Mabula alipiga marufuku hiyo Desemba 29, 2022 wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mtepera wilaya ya Kilwa mkoa wa Lindi wakati wa ziara ya kamati ya mawaziri nane wa wizara za kisekta ilipotembelea mkoa wa Lindi ikiwa ni utekelezaji wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975.

 

Uamuzi wa Dkt Mabula anayeongoza timu ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta unafuatia maelezo ya mkuu wa mkoa wa Lindi Bi Zainab Telack kuwa, baadhi ya wananchi wamekuwa na tabia ya kufanya shughuli za kibidamu kwenye maeneo ya hifadhi ya msitu wa Nyengedi na Pori  la Akiba la Selous wakati wana maeneo ya kutosha kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

 

Dkt Mabula amevitaja vijiji ambavyo wananchi wake wamekuwa na tabia ya kutoka maeneo yao na kwenda kufanya shughuli za kibinadamu katika eneo la hifadhi kuwa ni Chiodya B, Chiodya A, Mihango, Ntauna, Mnara, Mtakuja, Chikombe na Mkanga vilivyopo hifadhi ya msitu wa Nyengedi.

 

Vijiji vingine ni Mtepera, Zinga Kibaoni na Kikulyungu vilivyopo Hifadhi ya Pori la Akiba   Selous.

 

"Kijiji hiki cha Mtepera kina eneo kubwa ambalo halijatumika vizuri, mto matandu ni chanzo cha maji na unaanza kupoteza sifa kwa sababu tu shughuli za kibinadamu ziko karibu, wananchi wa eneo hawastahili kabisa kuwa karibu na vyanzo vya maji". Alisema Dkt Mabula.

 

Mapema wakati Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta walipokutana na uongozi wa mkoa wa Lindi, Mkuu wa mkoa huo Zainab Bi Telack alisema katika kushughulikia mogogoro ya matumizi ya ardhi, mkoa wake umebaini baadhi ya wananchi kuingia maeneo ya hifadhi na kufanya shughuli za kibinadamu na kuathiri ecolojia ya eneo la mto Matandu alioueleza kuwa ni mto muhimu na wenye faida kubwa kutokana na kuwa sehemu ya mto umaopeleka maji kwenye mradi mkubwa wa bwawa la Mwl Nyerere Rufiji.

 

Kwa mujibu wa Telack, mkoa wa Lindi umetenga maeneo kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo ufugaji ambapo aliwataka wananchi wa maeneo hayo kuanza kuchimba marambo na kubaki katika maeneo yaliyotengwa.

 

Kwa upande wao, Mawaziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt Pindi Chana, Naibu Waziri wa Maji Meryprisca Mahundi, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Khamis Hamza Chilo, Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega walisisitiza umuhimu wa wananchi wanaoishi karibu na hifadhi kuacha kuvamia na kufanya shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya hifadhi kwa kuwa shughuli hizo zinaleta athari za kimazingira ikiwemo kuharibu vyanzo vya maji.

 

Timu ya Mawaziri nane wa Wizara za kisekta inaendelea na ziara yake ya kutembelea mikoa mbalimbali nchini kwa lengo la kupeleka mrejesho wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya Matumizi ya ardhi katika vijiji 975.

 

No comments:

Post a Comment

Pages