HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 11, 2023

MIAKA 59 MAPINDUZI YA ZANZIBAR ACT WAZALENDO YATIA NENO

Hivi sasa ndani ya Visiwa vya Unguja na Pemba kumekuwepo na shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Tarehe 12 Januari 1964, huku kukiwa na shughuli mbali mbali za uzinduzi wa miradi ya maendeleo zinazowahusisha viongozi mbali mbali, kabla ya   Kilele cha Sherehe hizo hapo kesho.

Chama chetu kinawatakia kheri na mafanikio wananchi wote wa Zanzibar katika maadhimisho hayo ya miaka 59 ya Mapinduzi.  Aidha, kinawaomba wananchi na viongozi kuchukua kila hatua inayohitajika katika kuendeleza mshikamano, maelewano na maridhiano ya kitaifa kama msingi mkuu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Chama chetu kinapenda pia kukumbusha na kutanabahisha Malengo na Madhumuni ya Mapinduzi kama yalivyobainishwa na Sheria Namba 6 ya Mwaka 1964.  Sheria hiyo na matamko kadhaa ya muasisi wa Mapinduzi Marehemu Mzee Abeid Amani Karume yanaeleza wazi kwamba Mapinduzi ya kweli ni yale yanayolenga kumkomboa mwananchi kutokana na minyororo ya dhiki, unyonge, dhulma, ubaguzi, ukandamizaji, fitna na kuepukana na ukoloni wa kifikra, kupitia juhudi za makusudi za kujikwamua na kuyafikia maendeleo.  Aidha, kujenga mshikamano wa kitaifa, maelewano, kuondoa ubaguzi wa kiuchumi na kijamii na kujenga ustawi wa jamii.

Kwa msingi huo, Chama chetu kinapenda kumkumbusha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi kauli yaake aliyoitoa siku ya Tarehe 11 Novemba, 2020 wakati akifungua Baraza la kumi la Wawakilishi, kwamba Wananchi wetu wamechoshwa na siasa za uhasama, kuhubiri chuki na visasi ambazo hazibadilishi hali ya maisha yao kuwa bora zaidi. Wanataka matunda ya Mapinduzi na si simulizi za Mapinduzi na Muungano. Wanachotaka ni kustawi na kufaidika na matunda ya mapinduzi kwa usawa, bila upendeleo wala ubaguzi”.

Chama cha ACT- Wazalendo tunaamini kwamba, kama Nchi hatuwezi kuyafikia maendeleo, bila ya kuwepo azma njema ya kulinda heshima, uhuru, haki, usawa, umoja, mshikamano, utawala wa sheria, na maridhiano ya kweli ya kisiasa, yatakayopelekea ustawi bora wa jamii ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Chama cha ACT-Wazalendo tunaamini kuwa ili kuyatekeleza na kuyafanikisha hayo, tunawahimiza wananchi, viongozi, wapenda amani na kila anayeguswa na maendeleo ya Zanzibar, kuzingatia mambo yafutayo, kwa maslahi mapana ya Nchi yetu:

  1. Tuyatumie maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhamasisha maendeleo ya kweli ya Zanzibar, na kwa maslahi ya wananchi wote wa Unguja na Pemba, bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
  2. Kila mmoja wetu atekeleze wajibu wa kulinda, kuheshimu na kuendeleza Maridhiano ya Kisiasa ya Zanzibar yaliyopelekea kuwepo Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) iliyoasisiwa kwa ridhaa ya wananchi wenyewe na ridhaa hiyo kulindwa kikamilifu chini ya Katiba ya Zanzibar.  Ili kulinda, kudumisha na kuimarisha maridhiano na mshikamano uliopo chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Rais wa Zanzibar na viongozi wote husika hawana budi kusimamia utekelezaji wa yafuatayo kwa ukamilifu na kwa haraka:

 

                        i.         Kufanya mapitio ya haraka ya sera, sheria na taratibu zinazochangia kuongeza ugumu wa hali ya Maisha ambayo wananchi wote wa Zanzibar wanapitia katika kipindi hichi zikiwemo kodi, tozo, urasimu na ufisadi katika utendaji wa shughuli za umma;

                       ii.         Kuvunja kwa haraka mizizi ya unyanyasaji, udhalilishaji na uvunjaji wa haki za binadamu unaofanywa mara kwa mara na vikundi vinavyoratibiwa rasmi na baadhi ya taasisi za umma na ambavyo wananchi walitaraji vitakwisha chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya awamu ya 8 lakini bado vinaonekana vipo na vinatumika chini ya utawala wa Dkt. Hussein Mwinyi na mifano ya kutumika kwake ni pamoja na kumteka raia na kumtesa wakati wa Uchaguzi Mdogo wa Wadi ya Kinuni, kumteka na kumtesa kada wa CCM Bwana Baraka Shamte na kuwateka na kuwatesa vijana kadhaa hivi karibuni;

                      iii.         Kuondoa urasimu na ufisadi uliokithiri katika taasisi za umma ambako kunaongeza ugumu wa maisha kwa wananchi na kupunguza kasi ya maendeleo ya uchumi;

                     iv.         Kuharakiksha na kukamilisha upatikanaji wa Vyeti vya kuzaliwa na Vitambulisho vya Mzanibari Mkaazi kwa kila mwananchi mwenye haki.

                       v.         Kuimarisha mfumo mzima wa upatikanaji wa haki na kufanyia mabadiliko sheria mbali mbali ambazo misingi yake haikubaliki katika nchi abayo inafuata demokrasia ya Vyama vingi na inayozingatia na kuheshimu haki za binaadamu na utawala wa sheria

                     vi.         Kuunda upya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ili kufanya kuwa TUME HURU YA  UCHAGUZI

                    vii.         Kuandika Upya Sheria ya Uchaguzi Zanzibar (Zanzibar Elections Act) ili kuifanya izingatie matakwa na msingi wa demokrasia ya vyama vingi

                   viii.         Idara Maalum za SMZ kufanyiwa Marekebisho makubwa ili kuachana na kutumika kisiasa na kujiegemeza na Chama Cha Mapinduzi

                     ix.         Kufanyika marekebisho makubwa mfumo na Muundo wa utawala (administrative Structure and System) kuanzia katika ngazi za Mikoa, Wilaya, Wadi na Shehia.

                       x.         Kufanya Marekebisho Makubwa katika mfumo wa Utumishi wa Umma Zanzibar ili kukuza ufanisi katika kutoa huduma kwa umma na kuutenganisha Utumishi wa Umma na Siasa.

 

Mwisho kabisa, ACT-Wazalendo tunawatakia kila la kheri wananchi wote  katika harakati zao za maisha na tunawaomba waendelee kunga mkono juhudi za kujenga umoja na mshikamano wa Wazanzibari.

No comments:

Post a Comment

Pages