HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 08, 2023

WANAWAKE TANESCO, SUWASA SINGIDA WAPANDA MITI KUELEKEA KILELE CHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI


Wanawake watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida wakionesha furaha yao kabla ya kwenda kupanda miti kwenye chanzo cha maji cha Mwankoko kilichopo nje kidogo ya Manispaa ya Singida ikiwa ni shamra shamra kuelekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani, kesho Machi 08,2023. 

 

Na Dotto Mwaibale, Singida

 

WANAWAKE watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na wenzao wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA) katika kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 08, 2023, wamepanda miti katika chanzo za maji cha Mwankoko kilichopo nje kidogo ya Manispaa ya Singida ikiwa ni moja ya kazi ya upandaji miti ili kuimarisha uoto wa asili utakaosaidia upatikanaji wa mvua na hivyo kuimarisha vyanzo vya maji kwa ajili ya kuzalisha umeme mwingi.

 

Mbali na upandaji miti wanawake hao wa TANESCO wametoa msaada wa unga, mafuta ya kula, sabuni na vitu vingine kwa watoto yatima wa Kituo cha Upendo Home for Street Children, ikiwa ni shamrashamra kuelekea maadhimisho ya siku hiyo ambayo duniani kote yatafanyika kesho.

 

Zoezi hilo la upandaji miti limefanyika leo Machi 7, 2023 kwa kuwashirikisha wakuu wa idara wa taasisi hizo mbili za Serikali mkoani hapa. 

 

Akizungumza katika zoezi hilo la upandaji miti Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa  Shirika hilo, Lulu Silungwe alisema TANESCO imekuwa ikitegemea mvua inayotokana na miti kwa ajili ya kusambaza huduma ya umeme hivyo zoezi hilo la upandaji wa miti litasaidia kukabiliana na athari za kimazingira na mvua kuwa nyingi. 

 

“Tumekutana hapa leo na wenzetu kutoka SUWASA kwa ajili ya kupanda miti chanzo cha maji Mwankoko chini ya kauli mbiyu yetu isemayo Panda Miti, Mvua Ndi, Umeme Ndindindi ikiwa ni moja ya kazi yetu kuelekea maadhimisho ya kilele cha Siku ya Wanawake Duniani ambayo ni kesho” alisema Silungwe. 

 

Alisema mbali ya kupanda miti pia watawatembelea watoto Yatima wanaolelewa Kituo cha Upendo Home for Street Children, kwa ajili ya kuwapatia zawadi mbalimbali ikiwa ni kazi yao nyingine kuelekea maadhimisho hayo. 

 

Neema Ntandu ambaye ni mfanyakazi wa shirika hilo alisema wamepanda miti 150 ya aina mbalimbali na kuwa watahakikisha inakuwa na kuimarisha chanzo hicho cha maji cha Mwankoko.

  

Mwenyekiti wa Wanawake wa Shirika hilo Mkoa wa Singida, Asiatu Mnanura akizungumza wakati wa kutoa msaada kwa watoto wa kituo hicho alisema wamefurahi kuwatembelea ukizingatia kuwa wao ni wazazi hivyo waliona vizuri jambo hilo liwe ni sehemu ya moja ya kazi yao kuelekea maadhimisho hayo. 

 

Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa SUWASA, Fatina Mbaga alisema ni wajibu kwa kila mwana Singida kupanda miti kwa wingi ili kuhifadhi mazingira jambo litakalosaidi kuhifadhi mazingira na kuwepo kwa mvua nyingi na hivyo kuwa na maji ya kutosha. 

No comments:

Post a Comment

Pages