HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 31, 2023

Azam Tv, Power Brush Studios waja na Filamu ya Kisayansi ya EONII


Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Azam TV kwa kushirikiana na Power Brush Studios imetangaza Filamu yao ya kwanza ya Kisayansi ya EONII iliyotayarishwa nchini ambayo inalenga kuonyesha vipaji na uwezo mkubwa ndani ya tasnia ya filamu Tanzania.

Akizungumza wakati wa kuitangaza filamu hiyo leo Jijini Dar es Salaam Afisa Mwendeshaji wa Divisheni ya Utangazaji kituo Cha Azam Media Ltd Mohamed Yahya amesema kwamba uandaaji wa filamu hiyo umegharimu kiasi Cha Dola za Kimarekani laki mbili (200,000).

Yahya amesema kwamba Azam TV kama taasisi imekua na maono ya kuimarisha tasnia ya filamu Tanzania katika soko la kimataifa, hivyo Power Brush Studio Kwa kushirikiana na Azam TV zimetengeneza filamu hiyo ya EONII Kwa kutumia timu ya utayarishaji wa ndani yenye ujuzi mkubwa.

“Tumekusudia kuizindua rasmi filamu hii kwa kuonyesha katika kumbi za filamu maarufu kama Theatre Kwa kiingilio nafuu sana ambacho tutawatangazia ndani ya muda mfupi ujao na mikoa itakayopata fursa hii ni Arusha, Mwanza, Dodoma, Tanga na Dar es salaam pamoja na Visiwani Zanzibar ambayo ni mikoa inayopokea watalii wengi kwa sasa ” amesema Yahya.

Nakuongeza kuwa ” EONII ni mpango wa Azam Media wa muda mrefu ulolenga kuongeza umaarufu na Matumizi ya filamu za ndani sambamba na kukuza ukuaji wa tasnia ya filamu za ndani kama ambavyo tunaendelea kufanya katika michezo mingine kama soka , Masumbwi , riadha , pamoja na tamthilia za ndani.

Aidha amesisitiza kuwa filamu hiyo ya EONII imebeba hadithi ya kuvutia ya ugunduzi wa kisayansi katikati ya uhitaji wa nishati ya uhakika na ombwe kubwa la kukosekana kwake kunakozua taharuki katika jamii husika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Studio za Power Brush ,Eddie Mzale amesema kwamba timu yake imewekeza ubunifu na maarifa makubwa katika kuandaa EONII nakwamba wanajivunia Kwa namna filamu hiyo ilivyokamilika kuanzia ubora mpaka hadithi yenyewe.

“Tunaamini filamu hii sio tu itavutia watazamaji ulimwenguni kote lakini pia kama chachu ya ukuaji wa tasnia ya filamu Tanzania, EONII ni uthibitisho wa vipaji na uwezo wa ajabu ndani ya tasnia yetu ya ndani ambapo Kwa mara ya kwanza tunatengeneza roboti mwenye uwezo wa kupigana vita Kwa silaha Kali za moto” amesema Eddie



No comments:

Post a Comment

Pages