Mzee Jumaa Rico akimweleza matatizo yaliyopo katika hospital hiyo.
Mwenyekiti akimsalimia mmoja ya mama waliojifungua katika hospital hiyo.
Mganga Mkuu wa Hospital Mpya ya Wilaya ya Tanga Dkt. Stephen Mwandambo akisoma taarifa ya hospital.
Na Mashaka Mhando, Tanga
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Tanga Ustadh Rajabu Abdalahman Abdalah MNEC, amekutana na changamoto lukuki katika hospital mpya ya wilaya ya Tanga, ikiwemo barabara ya kuingilia, kutopitika.
Lakini pia hospital hiyo, miundombinu yake bado haipo vizuri kati ya wodi na wodi, haina jenereta endapo umeme utazima, taa za nje, upungufu wa vifaa tiba, upungufu wa watumishi na ukosefu wa gari la wagonjwa.
Mwenyekiti huyo anayefanya ziara ya siku tatu katika Jiji la Tanga, alielezwa kuwa ili uweze kufika katika hospital hiyo zipo barabara tatu ambazo kati ya hizo ni moja ndiyo inayopitika kwa sasa.
Hospital hiyo ya wilaya imejengwa katika kata ya Masiwani Shamba na barabara inayopitika ni ile inayotokea Kange Uzunguni.
Barabara ambazo hazipitiki kabisa kwa sasa kutokana na mvua zinazonyesha ni kutoka Mwahako na ile inayotoka Magomeni kupitia Njombe.
"Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM mimi nakaa nyuma ya hospital ili uje hapa inakubidi uzunguke Mbugani kwasababu hapa jirani kuna mto hatuwezi kuvuka," alisema Mohamed Self.
Kero nyingine ambayo imemshangaza Mwenyekiti ni halmashauri kutoa shilingi milioni 100 katika mapato yake ya ndani ili kujenga wodi ya watoto, wanaume na wanawake miezi mitatu iliyopita lakini hadi sasa fedha hizo hazijatumika kwasababu watu wa manunuzi hawajakamilisha mchakato wa kumpata mkandarasi.
"Halmashauri imetupa kiasi cha shilingi milioni 100 katika mapato yake ya ndani lakini mwezi wa tatu huu tangu tupatiwe bado mkandarasi hajapatikana," alisema Mganga Mkuu wa hospital hiyo ya wilaya Dkt Stephen Mwandambo.
Dkt Mwandambo pia alisema hospital hiyo ina watumishi 41 kati ya mahitaji ya watumishi 200 kwa kadirio la chini.
Alisema hospital hiyo iliyoanza kutoa huduma mwaka 2020, ilijengwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza ilitumia kiasi cha shilingi bilioni 1.8 na awamu ya pili ikapewa sh. 453,875,792.00.1
Akizungumza baada ya kuelezwa changamoto na kuitembelea hospital hiyo, Mwenyekiti alisema wananchi wa Jiji la Tanga wamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha kujenga hospital hiyo.
Alisema Chama cha Mapinduzi CCM wanao wajibu wa kuisemea serikali kutokana kazi nzuri inayofanywa na rais katika sekta mbalimbali hapa nchini na akawataka watendaji waende na kasi ya Rais Dkt Samia katika kuwaletea Maendeleo wananchi.
"Ndugu zangu wananchi serikali yenu ni sikivu italeta na kuongeza watumishi lakini pia italeta vifaa tiba ili muweze kupata huduma," alisema Mwenyekiti huyo.
Kuhusu miundombinu ya barabara na taa katika hospital hiyo, Meya wa Jiji hilo Abdulhaman Shiloh aliahidi kwa kushirikiana na TARURA watazikamilisha barabara hizo katika mwaka ujao wa fedha.
Alisema barabara ya kutoka Magomeni imekumbwa na changamoto ya baadhi ya nyumba ili kujenga barabara ya kiwango cha lami hadi hospital lazima ulipe fidia kwa nyumba 45 kiasi cha shilingi milioni 385 ambazo watazitenga katika bajeti ijayo.
No comments:
Post a Comment