RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza ujumbe wa viongozi mbalimbali na wananchi katika mapokezi ya ndege mpya kubwa ya mizigo aina ya B767-300F iliyonunuliwa na Serikali kwa ajili ya kusaidia usafirishaji wa haraka wa bidhaa za mazao na nyinginezo kwenda nje ya nchi.
Ndege hiyo kubwa ya kisasa yenye uwezo wa kubeba tani 54 za mizigo na kuruka kwa masaa 10 angani, inatarajiwa kuwasili nchini Tanzania Juni 3, 2023 katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam juu ya ujio wa ndege hiyo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema ndege hiyo ya mizigo B767-300F inatumia mafuta kidogo ukilinganisha na ndege nyengine za aina hiyo, yote ikiwa ni kupunguza gharama za uendeshaji na utoaji huduma.
"...Ujio wa ndege hiyo kutaleta unafuu kwa wakulima na wafanyabishara wa mazao ya mbogamboga, maua, nyama, Samaki, madini na kurahisha usafirishaji wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na Serikali pamoja na wafanyabiashara hususan madawa (pharmaceuticals).
Akifafanua zaidi alisema Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) inatarajia kuitumia ndege hiyo kuhudumia kusafirisha mizigo katika vituo vya kikanda na kimataifa kama Nairobi, Dubai, Mumbai, Guangzhou, Harare, Kinshasa na pia itakuwa inatoa huduma kwa kukodiwa na Wafanyabiashara mbalimbali kulingana na mahitaji yatakayojitokeza.
Prof. Mbarawa alisema kwa mujibu wa takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka Tanzania inazalisha wastani wa tani 10,471 za mazao ya samaki na nyama na wastani wa tani 11,200 za mazao ya maua, mbogamboga, na matunda. Na kwa mwaka zinazalishwa jumla ya Wastani wa Tani 24,971.
Alisema mazao hayo husafirishwa kwenda kwenye masoko ya nchi za Ulaya na Asia kama Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, Ugiriki, Hispania, Cyprus, Romania, Malta na India kwa kutumia usafiri wa anga. Aidha aliongeza mizigo inayosafirishwa kupitia katika viwanja vya ndege vya Tanzania kwenda katika nchi hizo ni wastani wa tani 420 kwa mwaka kati ya wastani wa tani 24,941.
"..Sababu za mazao hayo kusafirishwa kupitia viwanja vya nchi jirani ni kutokana na nchi hizo kuwa na ndege za mizigo zinazofanya safari zake kuunganisha miji hiyo na nchi za Ulaya na India ambazo ndizo walaji wakuu wa mazao yanayozalishwa Tanzania, Kutokuwepo kwa ndege za mizigo kutoka Tanzania kwenye masoko ya Ulaya kunachangia mazao yanayozalishwa Tanzania kusafirishwa kwa gharama kubwa kulinganisha na viwanja vya nchi jirani; hivyo ujio wa ndege ya mizigo ya ATCL kutawezesha mazao ya kilimo, mifugo na samaki kusafirishwa kwa bei nafuu kwenda katika masoko ya nje kutachochea ukuaji wa uchumi na kuhamisha Wafanyabiashara kuongeza uzalishaji kutokana na kuwa na uhakika wa usafirishaji wa mazao yao kwenda katika masoko ya kimataifa." Alisema Prof. Mbarawa.
No comments:
Post a Comment