HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 28, 2023

CCM ndiyo iliyodai Uhuru haiwezi kuwauza Watanzania

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Ustadh Rajab Abrahaman Abdalah MNEC.


 

NA MASHAKA MHANDO, Tanga

 

WATANZANIA wametakiwa kufahamu kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho kilichodai Uhuru wa Tanzania hivyo kwa namna yoyote ile hakiwezi kuiuza nchi, kilichofanyika katika bandari ya Dar es salaam ni uwekezaji unaolenga kukuza uchumi wa nchi.

Sambamba na hilo, Watanzania pia wametakiwa kukataa ghiliba na maneno ya uwongo yanasemwa na wanasiasa wa vyama vya upinzani kupotosha makubaliano baina ya serikali ya Tanzania na Umoja wa nchi za Kiarabu kupitia kampuni ya DP World.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Mabanda ya Papa kata ya Msambweni Jijini Tanga, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Ustadh Rajab Abrahaman Abdalah alisema maneno ya uwongo yanasemwa na wapinzani wakishirikiana na watu wanaojiita viongozi wa dini, yapuuzwe kwani yanahatarisha amani ya nchi.

Alisema serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan haiwezi kuiuza nchi kupitia mkataba huo ambao umetokana na utekelezaji wa ilani ya Chama ya mwaka 2020-2025 ya kuboresha bandari zilizopo hapa nchini ili kukuza uchumi wa nchi.

Mwenyekiti huyo alizungumza huku akisikitishwa na maneno yaliyosemwa na viongozi wa upinzani katika mkutano walioufanya Temeke Jijini Dar es salaam kwamba ni kukosa ajenda iliyosababishwa na CCM kutekeleza ilani yake kwa kasi kubwa.

"Wapinzani hivi sasa hawana ajenda dhidi ya CCM, wamebaki kumtukana rais, wakilala ni bandari wakiamka ni bandari. Ndugu zangu chama hiki katika serikali kina watu makini hakiwezi kuiuza nchi na CCM ndiyo iliyodai uhuru na kinajua umuhimu wake," alisema Ustadh Rajab.

Alisema hoja wanayotumia wapinzani kuhusu uwekezaji huo kamwe wasiitumie kwa ajili ya kutafuta kura katika mkoa wa Tanga, hawatapata kwa vile wananchi wanaielewa CCM na dhamira ya dhati aliyokuwa Rais Dkt Samia ambaye amepeleka kiasi cha shilingi bilioni 429 kwa ajili ya kuongeza kina cha maji katika bandari ya Tanga.

Mwenyekiti huyo alimpongeza na kumshukuru Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo na timu yake kuzunguka katika mikoa mbalimbali kuwaelimisha Watanzania kuhusu mkataba huo ambao wapinzani wanaukosoa wakijua maendeleo yatakayopatikana baada ya uwekezaji huo utaleta tija kubwa.

"Ndugu zangu wa Tanga uwekezaji unaofanyika haufanyiki katika bandari nyingine, bandari ya Tanga haimo, bandari ya Mtwara haimo wala bandari ya Kigoma haimo ni bandari ya Dar es salaam pekee tena ni katika sehemu ndogo siyo bandari yote," alisema.

Mwenyekiti alifoka akiwataka wananchi wawe makini kusikiliza mjadala huo kutoka kwa viongozi wa chama na setikali kwasababu makubalino hayo yamekuwa na makelele kuliko yale yaliyodumu kwa miaka 22 baina ya serikali na kampuni ya Ticks ambayo imemaliza muda wake.

"Kabla ya DP World kulikuwa na kampuni ya Ticks hakukuwa na kelele kama hizi kwa miaka 22 waliyokaa kwanini leo amepewa mwarabu kelele ni nyingi ni lazima mjiulize alipokuwa mzungu kulikuwa kimya ipo miradi wanapewa wachina nako pia kumetulia lazima mjue pia wanaleta udini ili kutugawa Watanzania tusikubali," alisema.

Alisema amani na utulivu uliopo hapa nchini ni jambo la msingi kwa Watanzania na wasione inaendelea kuwepo kwa bahati mbaya hapana ni mkakati madhubuti unaolindwa makusudi na serikali ya CCM kwa kila rais anayeshika madaraka kuilinda kwa kuwatendea mema wananchi.

Awali viongozi wa chama hicho akiwemo Mwenyekiti wa wilaya Meja mstaafu Hamisi Mkoba, katibu wa ccm wilaya Suleiman Sanko, Meya wa Jiji la Tanga Abrahaman Shilow, Katibu wa UVCCM Theresia Makyao na Mwenyekiti wa Uvccm mkoa wa Tanga Ramadhan Omari waliwataka wananchi wa Tanga, kupuuza maneno ya uwongo na kuiunga mkono serikali juu ya uwekezaji huo ambao utakuwa na tija kwa nchi.

Mwenyekiti wa UVCCM aliwataka viongozi wa CCM na wale waliokuwa kwenye serikali ambao hawaungi mkono ajenda ya mkataba huo ni vema wakakaa kimya kuliko kuchangia na kupotosha Watanzania akisema umoja huo na taarifa zao wataziweka hadharani.

No comments:

Post a Comment

Pages