HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 06, 2023

Mradi wa LNG kuzingatia maeneo matano muhimu


Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni akiangalia kifaa ambacho kinaonesha namna Mradi wa LNG utakavyokuwa.

Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau wa PURA Charles Nyangi, akimuelezea Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni kuhusu mwitikio wa watu kwenye bando lao ndani ya Sabasaba.
Mkurugenzi Mkuu wa PURA Mhandisi Charles Sangweni akizungumza na wasaidizi wake.



Na Selemani Msuya


IMEELEZWA kuwa utekelezaji wa Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG) unaotarajiwa kuanza hivi karibuni, utazingatia makubaliano ya mikataba matano.


Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Timu ya Majadiliano ya Serikali na Wawekezaji wa Mradi wa LNG, Mhandisi Charles Sangweni, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya 47 yaliyoendelea katika Uwanja wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.


Sangweni ambaye ni Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), amesema wamefanya mazungunzo tangu Novembaa 8,2021 hadi Mei 19, 2023 na kukubaliana mikataba mitano muhimu kwa kila pande na kwamba kwa sasa yapo katika hatua za maamuzi.


Mwenyekiti huyo amesema wamekubaliana kuwepo kwa Mkataba wa Nchi Hodhi (HGA), ambao umeanisha misingi ya uwekezaji,  ugawanaji na utekelezaji wa mradi wenyewe, ikiwemo uwajibikaji wa kila upande ambao ni Serikali, wawekezaji na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). 


“Mkataba wa pili ni unahusu Ugawanaji Mapato (PSA) ambao utaendana na mradi, mkataba wa tatu ni kuhusu ukodishaji ardhi ambapo mtambo utajengwa, kwani eneo hilo linamilikiwa na TPDC,” amesema.


Mhandisi Sangweni amesema mkataba wa nne unahusu namna wawekezaji watakavyoshirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) wakati wa usafirishaji LNG kwa kutumia meli kubwa kutoka nchi za Asia kama Japani na kwingineko.


Amesema mkataba wa tano ambao wamejadiliana na kukubaliana ni kuhusu ulinzi na usalama wa miundombinu ambapo jukumu hilo litasimamiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kama sheria za nchi zinataka.


Mkurugenzi huyo amesema katika mchakato huo wa makubaliano wameshirikisha taasisi zote kama TPDC, TPA, JWTZ, PURA, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bima, Uhamiaji na wengine.


  “Mradi huu ujenzi wake utagharimu shilingi trilioni 97, lakini taarifa zinaonesha kuwa uamuzi wa kuweka mtambo wa uzalishaji nchi kavu, Tanzania itaingiza zaidi shilingi trilioni 15 katika mfumo wa uchumi na wachumi wanasema Pato la Taifa (GDP) inaweza ikapanda hadi asilimia 8,” amesema.


Sangweni amesema wakati wa ujenzi wa mradi wanatarajia zaidi ya Watanzania 10,000 kupata ajira na baada ya kukamilika ajira 400 hadi 600 zitapatikana.


Amesema pia mradi huo utanufaisha sekta ya kilimo kwa kuwezesha watu kupata chakula, malazi, usafirishaji na nyingine ambazo huduma zake zitahitajika.


Mwenyekiti huyo amesema eneo ambalo linazunguka mtambo litakuwa maalumu kama ukanda wa kiuchumi kwa kujengwa viwanda ambavyo vitatumia gesi inayobaki kuzalisha na kutumika kwa maeneo ya karibu.


“Kimsingi suala la LNG kwa sasa lipo katika hatua mbalimbali za kukamilisha mazungumzo, ila makubaliano kama makubaliano tulimaliza Mei 19,2023,” amesema.
Kwa upande mwingine Mhandisi Sangweni amesema utafiti wa gesi na mafuta nchini umeanza kufanyika tangu miaka 1950 na hadi sasa wamechimba visima 96 na visima 44 ndivyo vimekutwa na gesi na 52 havikuwa na kitu.


Mkurugenzi huyo alisema katika visima 44 wamegundua gesi asilia zaidi ya futi za ujazo trilioni 57 katika maeneo ya Songo Songo mkoani Lindi, Mnazi Bay, Ntoria Mtwara na Bahari Kuu katika kitalu namba moja, mbili na nne, ambapo wanazalisha gesi asilia katika eneo la Songo Songo na Mnazi Bay ambayo husafirishwa kuja jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi huyo amesema gharama za uchimbaji wa kisima kimoja cha gezi ni zaidi ya shilingi bilioni 40 na maeneo mengine ni zaidi ya shilingi bilioni 80 na kwamba iwapo gesi inagundulika Serikali inapata mrabaha wa asilimia 12.5 kwa nchi kavu na baharini asilimia 5 hadi 7.5.


Amesema gesi asilia ambayo imepatikana ndiyo inazalisha umeme kwa asilimia 60, huku nyingine ikitumika kwenye mahoteli, majumbani na magari.


Mkurugenzi huyo alisema PURA ambayo imeanzishwa 2015 ina majukumu 18 ila wameyaweka katika makundi matatu, ikiwemo kumshauri Waziri wa Nishati kuhusu uendelezaji na utekelezaji wa miradi ya mafuta na gesi kwenye mkondo wa juu.


Amesema jukumu lingine kuu ni kusimamiamia na kudhibiti mradi wa LNG ambao unatarajiwa kuanza hivi karibuni na kukamilika 2030.

No comments:

Post a Comment

Pages