Na Mwandishi Wetu
WANANCHI wanaotembelea Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa sabasaba wameshauriwa kufika katika kituo cha Msaada wa Sheria ndani ya banda la Chuo Kikuu Mzumbe ili kupata msaada na ushauri wa kisheria katika changamoto mbalimbali zinazohitaji ufumbuzi wa kisheria.
Akizungumza Julai 4, 2023, Kaimu Rasi wa Ndaki ya Dar es Salaam Profesa Cyriacus Binamungu amewashauri kutembelea banda lao ili kujipatia huduma hiyo bila malipo na kutumia fursa ya maonesho hayo kupata msaada wa kisheria katika Nyanja mbalimbali zikiwemo; sheria za biashara, namna za kufungua na kuendesha biashara, pamoja na namna ya kufungua na kuendesha makampuni.
Aidha, Profesa Binamungu amesisitiza wananchi kupata elimu kuhusu umuhimu wa kuandika wosia kwenye mirathi kwani watu wengi wanafariki bila kuacha wosia na hivyo kuacha matatizo makubwa kwenye familia zao na mchakato wa kupata mirathi unakuwa ni mgumu.
“Familia nyingi zinakumbana na changamoto na migogoro mingi iwapo mmoja wa wanafamilia anapofariki bila kuacha wosia ili kuepusha migogoro na mchakato kuwa mgumu ni bora wanafamilia kuandika wosia mapema.
"Nawashauri wananchi wote kutembelea banda la Chuo Kikuu Mzumbe ili kuja kupata ushauri wa umuhimu na jinsi ya kuandika wosia’’ Amesema Prof. Binamungu.
Sambamba na hayo Prof. Binamungu amegusia upande wa sheria zinazohusu mambo ya kifamilia na kutoa rai kwamba watu waje kujifunza utaratibu wa kupata talaka na au mambo yanayohusiana na hayo kama matunzo ya watoto na sheria za ndoa kwa ujumla wake.
Kwa Upande wake Mhadhiri Msaidizi wa Kitivo cha Sheria na Mratibu wa Kituo cha msaada cha Chuo Kikuu Mzumbe, Wakili Benadetha Iteba amesema katika Maonesho ya Mwaka huu wamekuja na huduma mbalimbali za Msaada wa kisheria hivyo anawakaribisha wananchi wote wanaotembelea banda la Chuo Kikuu Mzumbe kwenda kujipatia elimu na ushauri wa kisheria bure katika maonesho hayo yanayoendelea mpaka Julai 13, 2023.
No comments:
Post a Comment