HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 06, 2023

Mkuu wa Wilaya Handeni aagiza Bati zilizonunuliwa kuchukuliwa sampuli kuthibitisha ubora wake TBS

 Na Mwandishi Wetu, Handeni

MKUU wa Wilaya ya Handeni, wakili Albert Msando, ameagiza kuchukuliwa sampuli za bati kwa ajili ya kupimwa na Shirika la Viwango nchini (TBS) ili kuthibitisha ubora baada ya kamati ya Fedha ya madiwani kushauri yasitumike kwa vile hayana ubora.

Mkuu wa wilaya hiyo katika taarifa yake aliyoitoa jana alisema kumekuwa na sintofahamu kuhusu bati zilizosambazwa na kampuni ya Great City Material Tanzania Limited ya Jiji Arusha.

Alisema anawashukuru na kuwapongeza wote ambao wanafuatilia na kusimamia miradi inayotekelezwa na serikali na kuona kasoro mbalimbali.

"Nawapongeza Madiwani wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Handeni Mji Mussa Abeid Mkombati kwa  kukagua na kutoa taarifa kuhusu ubora wa bati zilizosambazwa na kampuni ya Great City Material Tanzania Limited," alisema.

Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo Ofisi yake imechukua hatua ambapo Julai  2, 2023 alifika na kuona bati hizo ambapo alielekeza kuchukuliwa kwa sampuli za mabati hayo zikapimwe na TBS ili kuthibitisha ubora kama ambavyo Kamati ya Fedha ya Madiwani ilishauri.

Hivyo aliwaomba wote wawe na subira ili kukamilisha zoezi hilo na endapo itathibitika hazina ubora watahakikisha Mzabuni anawajibika na bati hizo hazitatumika.

Alisema kwa kuwa Mzabuni alitoa warranty ya miaka mitano itamlazimu kubeba gharama zote za kubadilisha bati hizo na ikithibitika zina ubora Mafundi wataendelea na ujenzi kama kawaida.

"Watu wa TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) wanatakiwa jambo hili walichunguze kwa makini sana haiwezekani ununue mabati kutoka kiwandani kwa bei ile," alisema.

Mabati hayo yamenunuliwa kwa bei ya Sh 43,700 kiwandani mkoani Arusha kwa kila moja na yapo zaidi ya 2,000 katika halmashauri hiyo na mengine zaidi ya hayo yamepelekwa halmashauri ya wilaya ya Handeni.

Pia madiwani hao walidai kuwa wamekuta kasoro katika misumari mfuko wa kilo moja  wamekuta robo kilo hamna.

No comments:

Post a Comment

Pages