Na Selemani Msuya
KAMATI ya Kitaifa ya Kuongoa Shoroba (NWCRC) imesema Serikali ipo katika mchakato wa kuandaa mpango makakati wa kuongoa shoroba 61 zilizopo, huku kipaumbele kikiwa ni kuanza na shoroba 20 zilizopo hatarini kupotea.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Lina Kitosi wakati akitembelea na kuona jitihada zinazofanywa na Shirika lisilo la Kiserikali la Mpango wa Kuhifadhi Tembo Kusini mwa Tanzania (STEP) kwa kushirikiana na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) Tuhifadhi Maliasili kurejesha Ushoroba wa Tembo Kilombero mkoani Morogoro.
Ushoroba huo unaunganisha Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa na Nyerere ambapo USAID Tuhifadhi Maliasili inashirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), kutoa habari zenye kuelimisha umuhimu na faida za kutunza na kuendeleza shoroba.
Alisema mwaka jana serikali iliunda kamati hiyo ambayo ina jukumu la kupitia shoroba zote 61 na kutoa mapendekezo kwa viongozi wa wizara husika namna ya kuzifanya ziwe endelevu.
Kitosi alisema kamati hiyo inayoundwa na watalaam kutoka wizara na taasisi mbalimbali, ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Ujenzi na Uchukuzi, taasisi na wadau wote wanaohusiana na uhifadhi na wanyama.
“Tulikutana mwaka 2022 kwa ajili ya kuandaa mpango kazi wa kuongoa shoroba na tutawasilisha kwa viongozi wa juu wa wizara husika, ili kutoka na msimamo mmoja wa kuokoa shoroba na hiki kinachofanywa na STEP ni darasa,” alisema.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Wanyamapori ambaye ni Katibu wa Kamati ya NWCRC, Dk. Fortunata Msofe alisema kamati hiyo inatekeleza mpango wa miaka mitano wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambao utahakikisha shoroba zinakuwa salama na endelevu.
“Baadhi ya shoroba zenye changamoto ni Kilombero, Kwakuchinja, Ngorongoro Serengeti, Ruaha Rungwe Kitulo, Selous Nyasa na nyingine,” alisema.
Alisema shoroba zinakabiliwa na changamoto ya kuongezeka kwa makazi na kilimo hivyo kupitia kamati hiyo watahakisha mkazo unawekwa kwenye shoroba 20 ikiwemo ya Kilombero ambayo STEP na USAID Tuhifadhi Maliasili na wadau wengine wanashirikiana kuiongoa.
Alisema iwapo kila mdau atashiriki kikamilifu kutekeleza majukumu yake asilimia kubwa ya shoroba zitaokolewa na kurejea katika hali ya awali.
Meneja wa STEP, Joseph Mwalugelo alisema ili kuhakikisha shoroba zinakuwa endelevu ni vema Serikali na wadau kujikita katika kutoa elimu kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment