HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 04, 2023

Serikali kujenga Bwawa la Yongoma

 Na Mwandishi Wetu, Same

SERIKALI imesema kupitia Bajeti ya mwaka 2023/2024, imepanga kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina kwa ajili ujenzi wa Bwawa la Yongoma lililopo wilayani Same mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na kuinua kipato cha wakulima.



Hayo yamesema na Naibu Waziri wa Kilimo, Antony Mavunde alipofanya ziara ya kikazi wilayani humo, kukagua maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji na miundombinu yake katika kata  za Ndungu, Miamba na Kihurio.

Alisema Rais Samia Suluhu Hassan amekipa kilimo kipaumbele cha juu, ambapo Bajeti ya mwaka 2023/2024 Serikali imetengea shilingi bilioni 970, kati ya fedha hizo zaidi ya shilingi bilioni 384 zimeelekezwa kwenye umwagiliaji.

Mavunde alisema Rais Samia amedhamiria kuinua kilimo ndio maana amewezesha Tume ya Taifa ya Umwagiliaji fedha za ujenzi wa mabwawa, skimu na visima nchi nzima ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao nchini.



“Tumesikia kilio cha wakulima wa Ndungu juu ya ukarabati wa skimu hii, katika bajeti ya mwaka 2023/24 tumetenga fedha za ukarabati na ujenzi wa Bwawa la Yongoma,” alisisitiza Mavunde.




Awali Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni na Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Anne Kilango-Malecela wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa namna inavyoendelea kuwakumbuka wananchi wa Same.

Walisema kupitia miradi hiyo ya umwagiliaji uzalishaji wa mazao utaongezeka na kukuza uchumi wa wananchi kwa kiwango kikubwa na kwamba kufuatia kazi hiyo nzuri ya Serikali wananchi  hawatamsahau Rais Samia na shukrani zao watazilipa mwaka 2025.


Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa alisema Serikali kupitia Bajeti ya mwaka 2023/24 watafanya ukarabati wa mifereji ya skimu ya Ndungu ambayo inatoa maji mto Yongoma ili kuhakikisha wakulima 3,000 wanaolima zaidi ya hekta 680 wananufaika.

“Pia tutaendelea na ujenzi wa mifereji ya maji katika eneo la Miamba na kusanifu Bonde la Mto Saseni ili wananchi zaidi ya 68,000 wanufaike na kilimo cha umwagiliaji,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages