HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 07, 2023

TUME YA KUREKEBISHA SHERIA KUANDAA MASHINDANO YA UANDISHI WA INSHA KWA WANAFUNZI VYUO VIKUU NCHINI


Katibu Mtendaji wa Tume ya kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) , Bw. Griffin Mwakapeje    akizungumza wakati wa Kikao cha Menejimenti ya Taasisi hiyo kilichofanyika leo Julai 6, 2023  katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za tume hiyo jijini Dodoma.

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

 

KATIBU Mtendaji wa Tume ya kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) , Bw. Griffin Mwakapeje amesema Tume ipo kwenye mchakato wa kutekeleza  Mpango wa kushirikisha vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini katika mashindano ya Uandishi wa Insha za masuala mbalimbali ya Kisheria na yenye changamoto katika jamii  ili waweze kushiriki na kuchangia katika utaratibu wa marekebisho ya sheria kwenye maeneo husika.

Maelezo hayo ameyatoa wakati wa Kikao Cha menejimenti ya Taasisi hiyo kilichofanyika leo Katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi za Tume hiyo ambapo ameeleza kwamba yapo matukio mbalimbali yanayoibuka Katika jamii yenye mueonekano wa kisheria ambapo zikiandikwa Insha zinaweza kuisaidia Tume kupata taarifa za kitafiti.

Amesema kazi hiyo ya Uandishi wa Insha kwa wanafunzi  itasaidia kuwajengea wanafunzi hari ya kufanya utafiti na kuiwezesha Tume kupata  taarifa mbalimbali zitakazofanyiwa kazi Kwa kina na wataalamuwa Taasisi hiyo, Jambo ambalo litaongeza ufanisi wa Tume na maboresho ya sheria.

Aidha ameeleza kwamba washindi wa Insha watapatiwa zawadi mbalimbali zikiwemo  fedha  taslimu, kuchapishwa kwa maandiko yao kwenye jarida la tume, pamoja na vyeti na kwamba zoezi hilo litaongeza  hamasa kwa wanafunzi kuwa wazalendo Katika nchi yao.

"Tutafanya makubaliano na vyuo mbambali hapa nchini kuhusu Uandishi wa Insha ili kuwa na uratibu mzuri wa zoezi hili ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wanafunzi kufanya utafiti wa masuala mbalimbali ya kisheria yanayogusa jamii ili  mwisho wa siku maandiko hayo yasaidie  kufanya maboresho ya Sheria husika.

Katika kikao hicho, Bw. Mwakapeje amewahimiza wataalam na watumishi kuongeza jitahada kwenye utekelezaji wa majukumu  na kuwataka wawe wabunifu ili kuyafikia malengo yao.

Kikao hicho kikiendelea.
Kikao kikifanyika.
Washiriki wakifuatilia kikao hicho.
Mmoja wa washiriki wa kikao hicho akichangia jambo.
 

No comments:

Post a Comment

Pages