HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 12, 2023

MRADI WA MAJI KAGENYI OMUKALINZI WANG'ARA RUWASA KYERWA YAPONGEZWA.

Meneja wa wakala wa maji na usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA Wilayani Kyerwa Shukrani Tungaraza akitoa taarifa ya mradi wa maji wa Kagenyi Omukalinzi Wilayani Kyerwa.

 

Na Lydia Lugakila, KYERWA

KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2023 Abdalla Shaib Kaim ameridhishwa na mradi wa maji wa Kagenyi Omukalinzi uliopo katika kitongoji cha Nyaiyanga katika Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera kutokana na ubora wa viwango vilivyozingatia thamani ya fedha kulingana na mradi ulivyo.

Kaim alitoa kauli hiyo Agosti 12, 2023  wakati akiwa katika mradi wa maji Kagenyi Omukalinzi muda mfupi baada ya kukagua, kutembelea na kuzindua mradi huo.

"Niipongeze Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia kwa kazi nzuri kupitia utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na miradi mikubwa ya maji yenye nia na lengo la kumtua Mama ndoo kichwani kupitia kuwasogezea karibu huduma ya maji Wananchi" alisema Kaim

Kiongozi huyo aliwapongeza Wakala wa maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilayani Kyerwa kwa kazi nzuri wanayoifanya pamoja na Viongozi wa Wilaya hiyo kwa kutoa huduma kwa Wananchi wake.

"Tunafurahi kuona Mwenge wetu wa Uhuru umepita na kuweka jiwe la msingi na mradi umeendelea vizuri hadi kufikia hatua hatua hii ya uzinduzi kazi kubwa imefanyika nimeridhika hongereni sana" aliongeza kiongozi huyo.

Akisoma taarifa ya mradi huo wa maji Meneja wa wakala wa maji na usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA Wilayani Kyerwa Shukrani Tungaraza alisema kuwa ujenzi wa miundo mbinu ya mradi huo ni miongoni  mwa miradi ya maji ambayo unatekelezwa na Ofisi ya meneja RUWASA Wilayani humo kupitia fedha za  program ya lipa kwa matokeo.

"Mradi huu umetekelezwa kwa kutumia wataalm wa ndani kwa utaratibu wa Force akaunti lengo la mradi likiwa ni kusaidia Wananchi kupata huduma ya maji kwa umbali usiozidi mita 400" alisema Tungaraza.

Meneja huyo aliongeza kuwa mradi utekelezaji wa mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 kufanyika kwa shilingi 261,200,000.00 na unategemea kuwanufaisha wakazi 3,000 waishio Kijiji cha Kagenyi ambapo pia utazinufaisha taasisi zilizopo jirani kama shule na Hospitali ya Wilaya pamoja na kupunguza  umbali mrefu wanaotumia Wananchi kwenda kutafuta maji.

Aidha Tungaraza alitoa shukrani kwa Rais Samia kwa kutoa Fedha zilizowezesha utekelezaji wa mradi huo huku akieleza kuunga mkono ujumbe wa Mwenge 2023, chini ya kauli mbiu isemayo Tunza Mazingira, Okoa Vyanzo vya maji kwa Ustawi wa Viumbe Hai na uchumi wa Taifa"

Hata hivyo kwa upande wao wanufaika wa Mradi huo akiwemo Henerco  Elnest Kaburakyage, Mwl Jason Joseph kutoka shule jirani ya kiingereza iitwayo Pamoja, na Sevelin Emanuel aliyejitolea eneo la kujenga mradi wameipongeza Serikali kwa kutoa Fedha ili mradi huo uendelee.

Walisema kuwa awali walipata changamoto ya maji kwani walitumia maji ya tinga tinga, maji ya chumvi ikiwa ni pamoja na kuyafuata umbali mrefu kwa kutumia usafiri wa magari na pikipiki huku wasiokuwa na uwezo wa kutumia usafiri wakishindwa kufanya shughuli zao na kufuata huduma hiyo mbali kwa mguu huku wanafunzi kukosa masomo kutokana na adha hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages