Muonekano wa Bandari ya Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
BANDARI ni moja ya eneo ambalo likitumika kwa usahihi na ufanisi linaweza kuleta mapinduzi ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kitamaduni kwa jamii husika.
Nchi ya Singapore, China, Senegali, Urusi, Qatar, India na nyinginezo zimewekeza nguvu kubwa kwenye bandari na matokeo yake yamekuwa makubwa kiuchumi na kijamii.
Tanzania ni moja ya nchi ambayo ina bandari rasmi zaidi ya 10 katika bahari na maziwa ambayo yanaizunguka nchini.
Eneo la bahari lililopo Tanzania ni zaidi ya kilomita 1,400 kuanzia Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, na Mtwara, ambapo unaweza kutengeneza bandari na kufanya biashara ya kupokea meli kubwa zenye shehena.
Pia Tanzania ina bandari katika eneo la Ziwa Nyasa, kuanzia Mbeya, Njombe hadi Ruvuma ambapo maeneo yote hayo yanajihusisha na shughuli za kiuchumi kupitia bandari.
Ziwa Tanganyika ambalo linahusisha Mkoa wa Kigoma na Katavi nalo lina bandari nyingi zinazotumuka kusafirisha mizigo kutoka ndani nan je ya nchi.
Halikadhalika Ziwa Tanganyika nalo linalohusisha Mkoa wa Kagera, Mwanza, Geita na Mara limekuwa likichangia pato la taifa kupitia bandari zake.
Ni kwa mantiki hiyo unaona na kutambua faida za bandari katika kuchangia pato la taifa na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Katika mazingira hayo ndipo inapokuja hoja ya nchi kutaka uwekezaji kwenye bandari, ili mchango wa sekta hiyo uweze kuongezeka mara dufu.
Katika hilo Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), imeweza kuwapa nafasi wawekezaji wakubwa kama Kampuni Kimataifa ya Kuhudumia Makontena Tanzania (TICTS), ambayo ilifanikiwa kwa kiasi chake katika kuongeza idadi ya mizigo inayopitia Bandari ya Dar es Salaam.
Matarajio ya Serikali na TPA kushirikisha sekta binafsi ni kuongeza shehena na mapato ya kodi inayokusanywa na TRA kutokana na mzigo unaopitishwa Bandari ya Dar es Salaam, ambapo mzigo huo umekuwa ukiongezeka kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita na kwa kuzingatia uwekezaji unaotarajiwa kufanywa na Kampuni ya Bandari ya Dubai (DP World) miaka 10 Ijayo
Shehena iliyohudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikiongezeka kwa asilimia 5.14 kwa mwaka. Ongezeko hilo ni kutoka tani milioni 12.55 za mwaka 2012/13 hadi tani milioni 18.41 za mwaka 2021/22.
Katika kupata maoteo, kiwango cha ukuaji wa shehena kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita cha asilimia 5.14, kimetumiwa kupata matarajio ya shehena kwa kipindi kijacho cha miaka 10 kuanzia mwaka 2022/23 hadi mwaka 2032/33. Katika kipindi hicho, shehena inatarajiwa kuongezeka kutoka tani milioni 18.41 mwaka 2021/22 hadi tani milioni 33.44 ifikapo mwaka 2032/33.
Matarajio ya ukuaji wa shehena kwa kuzingatia uwepo wa mwekezaji kwa mujibu wa Mkataba (IGA), uwekezaji wa DPW utahusisha maboresho ya eneo la bandari, eneo la kuhifadhia mizigo, mifumo ya uendeshaji wa bandari na uwepo wa mitambo na vifaa vya kutosha. Maboresho haya yanatarajiwa kuongeza shehena na mapato ya kodi inayokusanywa na TRA kutokana na mzigo unaopitishwa bandari ya Dar es Salaam. Maoteo ya ongezeko hili yanatarajiwa kutoka tani milioni 18.41 mwaka 2021/22 hadi tani milioni 42.6 ifikapo mwaka 2032/33.
Ni katika mazingira hayo umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi kwa miaka saba mfululizo wastani wa ongezeko la kodi inayokusanywa na TRA kutokana na shughuli za kibandari imebaki kuwa asilimia 36.52.
Malengo ya Shehena kwa kipindi kama hicho hayakufikiwa kama ilivyopangwa ambapo ukuaji wake umekuwa chini ya asilimia 10 (wastani wa asilimia 4.36 kwa mwaka). Hali hiyo ikiachwa kuendelea hivyo bila kufanya juhudi za makusudi kufanya mabadiliko, itasababisha nchi yetu kupata athari mbalimbali ikiwa ni pamoja na.
Wateja kukimbia bandari za nchini kutokana na ufanisi mdogo na meli kuchukua muda mrefu kushusha na kupakia mizigo; bidhaa zinazopita katika bandari zetu kuwa za ghali na hivyo, kusababisha kupeleka gharama kubwa kwa mlaji wa mwisho;
Pia tukishindwa kuwapa nafasi wawekezaji kama DPW mchango wa mapato ya kibandari kutoongezeka na hivyo kufanya nchi kuendelea kutumia mikopo ambayo ni ghali katika kuhudumia wananchi wake;
Aidha, taarifa zinadai kuwa iwapo tutaendelea kuvutana kuhusu ujio wa kampuni kama DPW na nyingine uwezo wa bandari ya Dar es Salaam utafikia ukomo wa kutoa huduma na kuwa na tija ifikapo mwaka 2025/26.
Kiuchumi
Upatikanaji wa fedha za kigeni na ajira Kutokana na athari hizo, Wizara inaona upo ulazima wa kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuboresha utendaji wa bandari zetu na kuingiza zaidi mapato nchini.
Iwapo Tanzania itaridhia mkataba wa IGA itaweza kunufaika mosi kiuchumi ambapo kwa kuwezesha ushirikishaji wa sekta binafsi wenye tija na utakaosaidia katika kupanua wigo wa shughuli za bandari na kuchangia ukuaji wa mapato ya Serikali na kuongeza fursa za ajira kwa watanzania;
Kuchochea sekta zingine za uzalishaji na viwanda kwa kuhakikisha bidhaa ghafi na zilizozalishwa zinafika kwa wazalishaji na walaji kwa wakati na kupunguza gharama za kufanya biashara pamoja na za usafirishaji kwenye mnyororo mzima wa usafirishaji kutoka kwa wazalishaji kwenda kwa mlaji wa mwisho;
Pia kupunguza gharama za bidhaa zinazoingizwa nchini kutokana na kuwa na gharama ndogo za bandari; na kuongeza fursa za Serikali kuwekeza katika maeneo mengine kutokana na rasilimali zitakazoonekana zimetokana na kutowekeza bandarini.
Kisiasa
Kuchangia katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi hususan katika kuongeza fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja katika sekta mbalimbali za kiuchumi na hivyo kuongeza pato la mwananchi mmoja mmoja; na kuimarisha uhusiano wa diplomasia ya uchumi na ushirikiano baina ya Serikali za Tanzania na Dubai.
Kijamii
Kuchochea upatikanaji wa huduma za kijamii kutokana na sera ya kurudisha faida kwa jamii (Community Social Responsibility- CSR).
Wiki ijayo tutaendelea kwa kuelezea changamoto zilizopo kwa bandari ya Dar es Salaam kwa sasa na kwanini ni muhimu kuipa sekta binasi kama DPW ili kuwekeza.
No comments:
Post a Comment