Na Selemani Msuya
WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mpango utakaowezesha wakandarasi wazawa kushiriki kwenye miradi mikubwa, huku akielezea kukerwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) na Bodi ya Wakandarasi (CRB), kushindwa kuchukua hatua kali wa wakandarasi wazembe.
Aidha, Bashungwa amewashauri wahandisi hasa vijana kuunda kampuni za ukandarasi na ushauri ili waweze kutekeleza miradi mikubwa ya serikali kupitia Program ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT Ujenzi).
Bashungwa ameyasema hayo wakati wa Maadhimisho ya miaka 21 ya Mpango wa Mafunzo kwa Wahandisi wahitimu (SEAP) ambapo zaidi ya wahandisi 300 wamekula kiapo cha utii baada ya kujengewa umahiri katika tasnia hiyo.
Alisema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuwainua wahandisi na wakandarasi, hivyo chini ya uongozi wake anapambana kuhakikisha mpango wa kuwawezesha wazawa unakamilika kwa wakati.
Waziri Bashungwa alisema lengo la wizara ni kuaona miradi yote ndani ya mikoa inatekelezwa na wakandarasi wazawam na hilo litafanikiwa baada ya mpango huo kukamilika kwa kuwa utaweza kuruhusu kugawana kwa vipande vya mradi.
“Napenda kutumia jukwaa hili kuwaambia wakandarasi wazawa mjiandae kutekeleza miradi mikubwa ambayo imekuwa ikitekelezwa na wageni, hili linawezekana iwapo mtapewa vipande vidogo vidogo, ila mkibebwa mbebeke sio Rais anawapigania halafu mnaenda kuharibu,” alisema.
Alisema miradi ya ngazi ya mkoa na wilaya inayotekelezwa na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala ya Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kwa mwaka inagharibu zaidi ya shilingi bilioni 850, hivyo fedha hizo zinapaswa kwenda kwa wakandarasi wazawa.
Kwa upande mwingine Waziri Bashungwa amezitaka ERB na CRB kuchukulia hatua kali wakandarasi wanaohatarisha maisha ya Watanzania kwa kujenga barabara bila kuzingatia viwango.
Pia amewataka wahandisi kuhakikisha wanalipia leseni zao za uhandisi kabla ya Marchi 31 mwaka huu huku akiwataka wazingatie taaluma katika utekelezaji wa miradi.
Waziri huyo aliwashauri wahandisi ambao wamekula kiapo kushirikiana kwa kuanzisha kampuni za ushirikiano ili waweze kupewa miradi.
“Tuanaamini kwa kufanya hivyo, kwanza utasaidia nchi kwa kuokoa fedha za kigeni na wakitengeneza nguvu ya taaluma hizi na kwa wale walio hitimu wanapaswa kuzingatia viapo,” alisema Bashungwa.
Aidha, Waziri huyo alisema amefanya mazungumzo na Benki ya Dunia (WB) na wafadhili wengi kuhakikisha miradi wanayofadhili inahusisha wakandarasi wazawa.
Waziri Bashungwa alisema Serikali inatambua juhudi za wahandisi kuleta maendeleo katika Taifa na wanafanyia kazi changamoto zinazokabili Mradi wa SEAP, huku akizitaka taasisi kama CRB, TANROADS, TARURA na nyingine kutoa fedha kusaidia.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Khadija Rajabu Khamis alisema SEAP ni program ya kuungwa mkono na kwamba Serikali ya Zanzibar itashirikiana nayo.
Mwenyekiti wa Bodi ya ERB, Mhandisi Wakili Menya Menye Manga alisema katika kuhakikisha SEAP inakuwa endelevu baada ya miaka 21 ya uwepo wake wanatarajia kuanzisha shule ya wataalam wa uhandisi.
Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Wanandisi, Mhandisi Benard Kavishe amesema hadi sasa ERB imesajili zaidi ya wahandisi 37,000 huku wanawake wakiwa ni asilimia 25 pekee, hivyo jitihada zao ni kuhakikisha idadi hiyo inaongezeka, ili kuwepo na usawa.
Nao wadau wa sekta ya ujenzi Mhandisi Mohammed Besta wa TANROADS, Mhandisi Victor Seif wa TARURA, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhandisi Revocutus Mativila, Mhandisi Hadija Ally wa TPSF na wengine wameweka wazi kuwa wataendelea kushirikiana na ERB ili kuwezesha vijana wa SEAP kupata kazi.
No comments:
Post a Comment