HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 29, 2024

Mchakato Dira ya Taifa kushirikisha makundi yote

 Na Selemani Msuya


TUME ya Mipango imesema itazingatia maoni ya wananchi na wadau wengine katika kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya miaka 25, inayoanza 2025 hadi 2050.


Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Ofisa Mkuu Mwandamizi wa Tume ya Mipango, Dk. Crispin Rwakitimbo wakati akitoa mada kwa wahariri wa vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2020 hadi 2025 na Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo 2025 hadi 2050.


DK Rwakitimbo amesema ushirikishwaji wa makundi yote katika kuandaa dira na mipango ya nchi kwa pamoja kunachochea maendeleo na kasi ya huduma za kijamii.


Amesema hatua ambayo Tanzania imefikia kwa miaka 25 ya dira ya kwanza imechangia mabadiliko makubwa katika sekta nyingi.


"Ibara ya 63 kifungu cha 3(C) kinaeleza majukumu ya Tume ya Mipango, hivyo tunataka kila mwananchi na wadau wote washiriki kwenye kutoa maoni juu ya namna ya kuitekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo kwa maslahi ya Taifa," amesema.


Amesema dira ya taifa ya Tanzania imezingatia dira ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Kusini mwa Kusini mwa Afrika (SADC), hali ambayo itawezesha kwenda kwa pamoja kiuchumi na kijamii.


DK Rwakitimbo alianzisha baadhi ya maeneo ambayo yamefanikiwa kwa kuwepo kwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2022 hadi 2025 ni elimu, kilimo, afya, miundombinu na nyinginezo.


"Mfano mwaka 2022 kutokana na kuwepo kwa dira nzuri tumeshuhudia utoshelezi wa chakula umefikia asilimia 125 kutoka asilimia 95, lakini pia tunaona wanafunzi kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari wanasoma bure na mengine mengi," alisema.


Ofisa Mkuu huyo alisema kupitia dira hiyo kwenye sekta imeshuhudia kupungua kwa vifo kwa kina mama wajawazito kutoka 760 2,000 hadi 238 mwaka 2020 na matarajio yao ni kupungua zaidi.


Pia amesema kupitia dira hiyo zaidi ya kaya milion 3 zimepata msaada kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), huku huduma zingine za kijamii zikiendelea kuboreka.


Amesema kwa mafanikio ambayo yamepatikana kwa dira ya kwanza, wanaamini wakishirikishwa wananchi na wadau wengi dira ijayo itaweza kuleta mabadiliko makubwa zaidi.


DK Rwakitimbo amesema wanaamini wahariri na waandishi wa habari wakishiriki kikamilifu jamii itapata taarifa sahihi na kuwe sehemu ya utekelezaji.


"Tumejipanga kwenda kwa wadau wote yaani wananchi, asasi za kiraia, vyama vya siasa na wengine ili waweze kutoa maoni yao na nchi iweze kutekeleza yale ambayo watu wake wanataka," amesema.


Mkuu huyo amesema Tanzania inaweza kupiga hatua kwenye sekta zote iwapo kila mdau atashiriki kwa vitendo.


Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ameishauri Tume ya Mipango kushirikisha waandishi wa habari kuanzia hatua ya awali ya mchakato wa uandaaji wa dira ya taifa na sio kuja kwao wakati wa hatua za mwisho.


Aidha, Balile ameishauri tume hiyo kujifunza katika nchi zingine namna ya kuandaa mipango na utekelezaji wake, hali ambayo itachochea mafanikio kwa haraka.


"Mimi napenda kuwaomba tume muwe mnatushirikisha tangu mapema kwenye michakato ya dira na mipango mingine, ili tuondokane na kutoa kutoa taarifa kwa ufinyu," amesema.


Kwa upande wa wahariri wengine wamesisitiza ushirikishwaji kama nguzo muhimu ya kwenda kwa pamoja katika mambo yanayohusu maslahi ya nchi.



No comments:

Post a Comment

Pages