HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 28, 2024

BENCHIKHA AAPA KUIPELEKA SIMBA NUSU FAINALI

NA JOHN MARWA


KOCHA Mkuu wa Klabu ya Simba, Abdelhak Benchikha ameahidi kuipeleka klabu hiyo hatua ya nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika CAF CL ambapo kesho anakiongoza kikosi chake kumenyana na Miamba ya Afrika na Mabingwa watetezi Al Ahly ya Misri.



 Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Benchikha amesema amekiandaa vizuri kikosi chake kuelekea katika mchezo huo.


 Amesema vijana wake wapo tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya Al Ahly na wanahitaji kupata mabao mengi nyumbani, ili kujitengenezea mazingira mazuri kufuzu nusu fainali.


"Kuna tofauti kubwa nilipocheza dhidi ya Al Ahly nikiwa na US Alger na mchezo ule ulikuwa tofauti na huu. Ule ulikuwa mchezo mmoja tu, lakini sasa tunaenda kucheza michezo miwili, ambayo lazima tushinde ili kufuzu," amesema Benchikha.


Amesema, Al Ahly ni timu kubwa lakini lengo lake ni kuhakikisha anaivusha Simba kwa mara ya kwanza kuelekea hatua ya nusu fainali.


"Lengo tulilojiwekea hapo mbele ni kufika nusu fainali na hatuwezi kufika bila kushinda mchezo wa robo fainali. Al Alhy ni timu kubwa, tunaiheshimu lakini lazima tutumie vizuri uwanja wetu wa nyumbani, " amesema Benchikha.


Nae Nahodha Msaidizi wa Simba SC, Shomari Kapombe amesema wameandaa surprise kubwa kwa mashabiki katika mchezo huo huku akibainisha kuwa wana imani wataenda kupata matokeo chanya kesho Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.


Amesema  wamekuwa na wakati mzuri wa maandalizi tangu walipokuwa Zanzibar, hivyo kikosi hicho kipo kamili kupambana katika hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).
"Kwa niaba ya wachezaji wenzangu ninaawaambia mashabiki wa Simba kuwa waje, tumejiandaa kuonesha mchezo mzuri na kushinda mechi," amesema Kapombe.

No comments:

Post a Comment

Pages