HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 17, 2024

Sekta binafsi yasifu utekelezaji wa Mkumbi

Na Mwandishi Wetu

SERIKAL imepongezwa kwa utekelezaji wa mapendekezo ya sekta binafsi kupitia vikao na mikutano ya Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) ambapo sekta binafsi imekiri kupatikana kwa mafanikio makubwa    Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Mkumbi) ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan.


Akizungumza mara baada ya kikao cha 37 cha Kamati Tendaji cha TNBC jana, Katibu Mkuu Kiongozi ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Moses Kusiluka amesema sekta binafsi imeridhishwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali ya awamu ya sita katika kuboresha na kuweka mazingira na wezeshi ya uwezeshaji na ufanyaji biashara hapa nchini.



“Ni faraja kwetu kupata mrejesho chanya kutoka sekta binafsi  kwani inaleta afya sambamba  na kuonyesha dhamira ya kweli kuwa serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuleta mageuzi ya kiuchumi sambamba na kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji,” amesema Dk Kusilluka.

Mwenyekiti huyo amesema serikali imeshaondoa tozo mbalimbali ambazo zilikuwa kero kwa ustawi na ukuaji wa biashara hapa nchini kwa hayo yote ni matunda ya kazi ya Baraza la Taifa la Biashara.

Aidha, Dk Kusiluka amelipongeza Baraza kwa kazi nzuri wanayoifanya  ikiwemo kusimamia na kuhakikisha vikundi kazi vyake ambavyo makatibu wakuu ndiyo wenyeviti wa vikundi kazi hivyo.

Amesema vikundi kazi vimefanya kazi nzuri ikiwemo kujadiliana  na hatimaye kuja na  mapendekezo yanayowasilishwa kwenye kikao cha  kamati  tendaji kabla ya kupelekwa kwenye mkutano  wa Baraza  mwishoni mwa mwezi mei au Juni mwanzoni ambapo Rais ndiye mwenyekiti wake.

“Miaka mitatu ya uongozi wa Awamu ya Sita chini ya  Rais Samia  imeweza kuboresha na kuimarisha mazingira ya ufanyaji  biashara na uwekezaji  nchini ikiwemo kuchochea ukuaji wa sekta binafsi,” alisema Dkt. Kusiluka.

Naye Mwenyekiti Mwenza ambaye pia ni Mwenyekiti wa Sekta Binafsi nchini (TPSF) Angelina Ngalula ameipongeza serikali kwa kufanya maboresho makubwa na kufanikishwa utekelezaji Mkumbi.

 

”Serikali inapaswa kuendelea kutoa elimu zaidi kwa umma na wadau mbalimbali ili waweze kuelewa namna Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Mkumbi) unavyofanya kazi kwani utasaidia kuondoa mkanganyiko baina ya wafanyabiashara na sekta ya umma,” alisisitiza Ngalula.

 

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TNBC Dk Godwill Wanga amesema kuwa kikao hicho kimeangazia zaidi utekelezaji wa maazimio ya kikao cha 36 cha kamati tendaji ambapo jitihada kubwa zimechukuliwa katika utekelazaji wa maazimio hayo yenye lengo la kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini.

Aidha Dk Wanga amesema  moja ya ajenda   kubwa iliyojadiliwa ni pamoja na kuunganisha mifumo ya  serikali ili weze kusomana   na hivyo kujenga uchumi wa kidijiti utakao chochea na kuongeza tija katika uzalishaji na utoaji huduma  nchini.

“Mapinduzi ya  uchumi wa kidijiti  utatoa  mchango mkubwa katika kukuza  pato la mwananchi mmoja mmoja na taifa kiujumla sambamba na  kuchagiza maendeleo na ukuaji wa sekta nyingine za maendeleo na uchumi,” amesema Dkt Wanga.

Dk Wanga amesema kikao hiko  kimeelekeza maswala yote ya udhibiti yahakikishe yanadhibiti zaidi changamoto kuliko kuwadhibiti  wazalishaji ili kutoathiri ukuaji wa uchumi sambamba na    kufanya kazi kwa karibu  na sekta binafsi  ili iweze kuzalisha na kuchangia kikamilifu katika kukuza pato la Taifa.

No comments:

Post a Comment

Pages