HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 13, 2024

Serikali yaanza Ufungaji wa Kamera Magerezani

 

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo (wanne kulia)  akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa juu wa Jeshi la Magereza katika Makao Makuu ya jeshi hilo yaliyopo Msalato katika ziara hiyo ya kujitambulisha na kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na jeshi hilo,ziara hiyo imefanyika leo jijini Dodoma. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

 

Serikali imeanza  Ufungaji wa Kamera maalumu(CCTV) katika maeneo mbalimbali yanayozunguka magereza lengo ikiwa ni Uboreshaji wa Huduma za ulinzi na usalama  pamoja na kwenda na dhana nzima ya sayansi na teknolojia katika utoaji na ufuatiliaji wa huduma kwa wadau mbalimbali wanaoshilikiana na Jeshi la Magereza ikiwemo Jeshi la Polisi na Mahakama.

 

Hayo yamesemwa leo na Naibu Kamishna wa Jeshi la Magereza, Jeremia Katungu wakati akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Daniel Sillo wakati wa mkutano uliohusisha Uongozi wa juu wa jeshi hilo,Maafisa,Askari na watumishi raia  huku akitaja baadhi ya mikoa ambapo kamera hizo zimefungwa.

 

‘Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuliwezesha jeshi katika maeneo mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake, baadhi ya maeneo hayo ni ununuzi wa vifaa vya ulinzi na usalama katika maeneo yanayozunguka magereza kwa nje   ambapo kwa sasa zoezi la usimikaji wa vifaa hivyo kwa sasa unaendelea katika maeneo ya magereza ya Maweni, Karanga, Moshi, Lwanda na Tabora’.alisema.

 

Ameyataja maeneo mengine yaliyoboreshwa na serikali ya awamu ya sita kuwa ni vyombo vya usafiri,ajira,upandishwaji vyeo kwa askari na maafisa ambapo hadi sasa  jumla ya ajira 662 ziko katika mchakato wa usaili huku upandishwaji vyeo mpaka sasa askari na maafisa 4111 wamepandishwa vyeo.

 

Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Daniel Sillo amewataka Askari wa Jeshi la Magereza kuwa ni nidhamu katika utendaji wao wa kazi ili kujiepusha na tuhuma mbalimbali ambazo zitalichafua jeshi huku akimpongeza Rais Daktari Samia Suluhu Hassani kwa msaada anaotoa kwa vyombo vya ulinzi na Usalama likiwemo Jeshi la Magereza.

 

‘Sifa kubwa ya askari ni nidhamu,nidhamu hiyo inapaswa kuanzia ndani ya jeshi mpaka nje,nawaomba muendelee kuboresha nidhamu kazini ili kuboresha mahusiano yenu pamoja na viongozi wenu jueni mheshimiwa Rais anawategemea sana katika utoaji wa huduma na maelekezo yake ni kuwa Tume ya Haki Jinai ilishatoa mapendekezo sasa yafanyiwe kazi ili kuondoa baadhi ya changamoto ikiwemo msongamano wa wafungwa magerezani’ alisema Naibu Waziri.

 

Naibu Waziri Daniel Sillo ameaza ziara rasmi katika vyombo vya ulinzi vilivyopo ndani ya wizara baada ya muda mfupi kuteuliwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuhudumu katika nafasi hiyo.

 

No comments:

Post a Comment

Pages