HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 15, 2024

TBS yavuka lengo utoaji Leseni kwa Wazalishaji wa Ndani na Ukaguzi Bidhaa za Nje




Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS ) Dkt. Athuman Ngenya, akizungumza wakati wa kikao kazi cha Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Wahariri wa vyombo vya Habari kilichoratibiwa na Ofisa ya Msajili wa Hazina (TR) na kufanyika leo Aprili 15, 2024  jijini Dar es Salaam.

 

NA MWANDISHI WETU

 

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limetangaza mafanikio iliyopata katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo kuvuka lengo kwa asilimia 105 katika utoaji leseni za ubora wa bidhaa za ndani na asilimia 99 ya ukaguzi wa bidhaa za nje ya nchi.

 

TBS imeenda mbali kwa kufichua kuwa siri ya mafanikio yao katika kipindi hicho ni ushirikiano na taasisi nyingine za Serikali, zikiwemo TRA, FCC, TAMISEMI, Jeshi la Polisi, pamoja na vyombo vingine vya usalama katika kufanya ukaguzi ili kubaini bidhaa zisizokidhi matakwa ya viwango na kuchukua hatua stahiki.

 

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Athuman Ngenya, licha ya kufafanua mafanikio katika maeneo hayo, alieleza pia kuwa shirika limefanikiwa kusogeza karibu na wananchi huduma kwa kujenga maabara za kanda na zile za Mikoa ya Kimkakati nchini.

 

“Katika kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wazalishaji kwenye eneo la Uandaaji wa Viwango, kwa miaka mitatu hii, jumla ya viwango 1,721 vya kitaifa viliandaliwa, sawa na asilimia 101.2 ya lengo la kuandaa viwango 1,700. Viwango ambavyo viliandaliwa katika nyanja mbalimbali.

 

“Aidha, Serikali kwa kupitia TBS imekuwa ikitenga zaidi ya Sh. Mil. 250 kwa dhumuni la kuhudumia wajasiriamali wadogo bila ya malipo yoyote, ambako katika kipindi hicho jumla ya leseni za ubora wa bidhaa 2,106 zilitolewa kwa wazalishaji mbalimbali wa bidhaa hapa nchini sawa na asilimia 105.3.

 

“Hapo tulivuka lengo la kutoa leseni 2,000 na kizuri zaidi ni kwamba kati ya leseni hizo, jumla ya leseni 1,051 zilitolewa bure na kwa wajasiriamali wadogo,” alibainisha Dk. Ngenya katika wasilisho lake hilo lenye zaidi ya kurasa 30.

 

Dk. Ngenya akaongeza kuwa: “Katika kuhakikisha soko linakuwa na bidhaa zenye ubora, kwa kufanya kaguzi za bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini na kwa miaka mitatu hii, jumla ya leseni za ubora wa bidhaa 2,106 zilitolewa kwa wazalishaji mbalimbali wa bidhaa hapa nchini sawa na asilimia 105.3 ya lengo la kutoa leseni 2,000.

 

“ Na katika ukaguzi wa bidhaa zinazotoka nje ya nchi, TBS ndio yenye mamlaka ya kudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini kwa kutumia mfumo wa Pre-Shipment Verification of Conformity to Standards (PVoC) pamoja na kufanya ukaguzi pindi bidhaa zinapowasili nchini (Destination Inspection).

 

“Sasa kupitia ukaguzi huo, katika kipindi cha miaka mitatu, jumla ya shehena 100,851 kabla hazijaingizwa nchini (sawa na asilimia 99 ya lengo la kukagua shehena 102,083) na jumla ya bidhaa 151,570 kutoka nje ya nchi, zilikaguliwa baada ya kufika nchini sawa na asilimia 77 ya lengo la kukagua bidhaa 197,417,” alifafanua.

 

Dk. Ngenya alibainisha ya kwamba, katika kusogeza huduma karibu na wananchi TBS aidha imejenga ama inaendelea na ujenzi wa Maabara Katika Mikoa ya Kimkakati, ikiwemo ujenzi unaoendelea wa Makao Makuu ya Shirika na Maabara (Viwango House - Dodoma).

 

“Maabara hii itahudumia mikoa mitatu ya Kanda ya Kati ambayo ni Dodoma, Singida na Tabora, pamoja na mikoa mingine ya karibu. Kadhalika, shirika linatarajia kuanza ujenzi wa maabara ya kisasa katika Kanda ya Ziwa (Mwanza) na Kanda ya Kaskazini (Arusha).

 

“Maabara ya Kanda ya Ziwa inatarajiwa kuhudumia mikoa sita ya Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu, wakati maabara ya Kanda ya Kaskazini inatarajiwa kuhudumia mikoa minne, ambayo ni Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara,” alifafanua Dk. Ngenya.

 

Katika kuongeza na kuimarisha Ofisi za Kanda, Dk. Ngenya alisema TBS limefanikiwa kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia Ofisi za Kanda saba, ambazo ni Kaskazini (Arusha), Kusini (Mtwara), Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Magharibi (Kigoma), Kanda ya Ziwa (Mwanza), Kati (Dodoma) na Mashariki (Dar es Salaam).

 

“Kanda hizi zina ofisi katika mipaka ya nchi, bandari pamoja na Viwanja vya Ndege,” alibainisha Dk. Ngenya na kuongeza ya kuwa TBS limetengeneza Mifumo ya Kielektroniki inayotumika kutoa huduma zake, ambayo imewezesha wateja kupata huduma za shirika popote walipo kwa wepesi na haraka.

 

Katika hitimisho lake, Dk. Ngenya aliweka ahadi kwamba TBS itaendelea kuwa bega kwa bega na Serikali kutekeleza azma ya kuwezesha ufanywaji wa biashara nchini utakaoendana na kuinua viwanda kwa kusimamia ubora wa bidhaa, kulinda usalama wa mlaji, sambamba na kusimamia Mapato ya Serikali.


No comments:

Post a Comment

Pages