HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 27, 2024

VIJANA WALISHUKURU SHIRIKA LA PLAN INTERNATIONAL


Mratibu wa shirika Yes Tanzania linalofadhiliwa na Plan International, Shaban Ramadhan akitoa mafunzo kwa vijana walionufaika na Plan International.


NA DENIS MLOWE, SUMBAWANGA

BAADHI ya vijana wa Kata ya Ilemba wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa wamelishukuru shirika la Plan International kwa kuweza kuwasaidia kupata elimu ya fani mbalimbali ambazo zimewasaidia kujikwamua kiuchumi.

Wakizungumza kwenye kikao cha kujadili mafanikio mbalimbali baada ya kuwezeshwa na Pan Intenational vijana hao walisema kuwa wamefanikiwa kufungua ofisi zao ambao zimewakomboa kiuchumi mara baada ya kupewa elimu katika vyuo mbalimbali na shirika hilo.

Mmoja ya vijana hao, Vicent Luguya alisema Plan International kupitia mradi wa bingwa kuzuia mimba katika umri mdogo wa licha ya kuwa kinara wa kutoa elimu ya kuzuia mimba kwenye kata hiyo amefanikiwa kufungua karakana ambayo inajihusisha na utengenezaji wa mageti na ofisi ya steshenari ambao imekuwa mkombozi mkubwa katika maisha yake.

Alisema kuwa alipata fursa ya kupata mafunzo kupitia mradi mara baada ya kumaliza alirudi kwenye kata yao ya Ilemba na kuweka vikao mbalimbali vya majadiliano na vijana watu mbalimbali wa kata hiyo .

Luguya alisema kuwa mafunzo hayo yaliwasaidia mabinti wengi kuweza kujitambua na kuingia kwenye elimu za fani mbalimbali ikiwemo ususi, ushonaji na ufundi umeme, ambapo wengi wamefanikiwa kufungua ofisi zao kwa kuwezeshwa na shirika la Pan International.

Naye Elizabeth Simboye alisema kuwa kwa upande wake ameweza kujitambua kwa kiasi kikubwa na kuweza kupata manufaa kupitia mradi huo ukilinganisha na mabinti wa rika lake ambao hawajapata elimu ya mimba za utotoni na wengi wao kuishia kuolewa na kupata mimba bila kutarajia.

Aliongeza kuwa bila Pan International kufika katika kata hiyo angekuwa ameshaolewa na kuwa na watoto lakini kwa sasa amekuwa msaada mkubwa kwa familia kutokana na kuanzisha biashara ya ushonaji ambayo imekuwa mkombozi kwa familia baada ya kusaidia mashine ya kushona na shirika la Plan International

Elizabeth ametoa wito kwa wahisani kuweza kulisaidia shirika hilo ili liweze kuendelea kuwepo katika kata hiyo kwani limekuwa msaada mkubwa kwa mabinti kuepukana na mimba za utotoni kwa kuwapa elimu ya bure kabisa na misaada ya vifaa mbalimbali vya kufanyia kazi na kuitaka serikali nayo kuunga mkono juhudi za Plan International.

Kwa upande wake Mratibu wa shirika Yes Tanzania linalofadhiliwa na Plan International, Shaban Ramadhan alisema kuwa kama shirika  lilitambua viashiria mbalimbali ambavyo vinasababisha mimba za utotoni kwenye kata hiyo kama umasikini, elimu duni, shinikizo rika, uelewa mdogo wa jamii kuhusu sheria zinazosimamia masuala ya mahusiano ya watoto na wanafunzi, ukatili na usawa wa kijinsia.

Alisema kuwa kutokana na hizo Plan International ilivutiwa na ndio sababu ya kuja kupambana changamoto katika mkoa wa Rukwa hususani katika kata hiyo ya Ilemba na nyingine ambazo mradi unafanya kazi mkoani hapa na kuamua kufanya kazi na wadau ambayo ni mashirika ya Yes Tanzania, rafiki na kugawana afua zote tano kwenye maeneo mbalimbali..

Alisema kuwa changamoto nyingine zinazoikumba jamii hususani mabinti wadogo ni malezi hafifu, mila desturi na imani zinazomkandamiza mtoto wa kike, kuporomoka kwa maadili katika jamii, na kutokuwajibika kwa wazazi na viongozi katika ulinzi wa watoto wa kike.

Naye Meneja wa Mradi wa Kupinga Mimba na Ndoa za Utotoni kupitia shirika hilo linalofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Norway (Norad), Kisasu Sikalwanda alisema kuwa baada ya utafiti wa muda mrefu walikuja Rukwa kusaidiana na serikali kukabiliana na changamoto ya mimba za utotoni kwani hali haikuwa nzuri kwenye jamii.

Kwa kushirikiana na Shirika la Yes Tz, Rafiki SDO, Lusudeo, PDF na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Chala, Sikalwanda anasema Plan International inatekeleza afua tano zinazolenga kuusaidia mkoa huo kuhakikisha ifikapo mwaka 2025, tatizo la mimba na ndoa za utotoni linakuwa historia.

Anataja moja ya afua hizo kuwa ni ile inayolenga kuhakikisha mtoto wa kike anakwenda shule kwasababu Shule inasadia kumzuia na vishawishi vya mimba au ndoa kwasababu ya sharia, miongozo yake na mikataba mbalimbali ya kimataifa.

Anaongeza kuwa miaka minne ya mradi huo kutekelezwa kuna mabadiliko mengi yametokea ikiwemo  kupunguza utoro wa wanafunzi wa kike ukiwemo ule unaosababishwa na masuala yanayohusiana na hedhi unapungua huku na suala la mimba na ndoa za utotoni nazo zikipungua kwa kiasi kikubwa.

Alisema kuwa mradi huo unawafikia vijana wa rika balee wa kati ya miaka 10 na 24 ndani na nje ya shule katika wilaya ya Nkasi, Kalembo na Sumbawanga Vijijini kwenye kata ya Ilemba.

No comments:

Post a Comment

Pages