HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 23, 2024

Wanawake wanaopitia changamoto za kiuchumi wapewa mafunzo

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Macho kwa Jamii, Theresia Lihanjala (kulia), akizungumza jambo Wanawake wakifuatilia jambo kwenye mafunzo ya kujitambua na afya ya uzazi, ili wasiwe tegemezi.



Na Mwandishi Wetu


WANAWAKE wanaopitia katika changamoto za kiuchumi, wamepatiwa mafunzo ya kujitambua pamoja na afya ya uzazi, ili wasiwe tegemezi, waweze kufanya biashara zao kwa umakini.

Akitoa mafunzo hayo, Hilda Dadu amesema wanafundisha masuala ya ujasiriamali kwa wanawake hao, lengo likiwa ni kuwasaidia kujitegemea na kuachana na utegemezi.

 “Mabinti wengi ama kwa sababu wengi wanatoka katika familia duni zile familia hali ya maisha inawafanya wale mabinti kwenda kwenye masuala ya kutaka kuwa na vitu lakini ili apate kitu hujiingiza kwenye masuala ya  mahusiano, wakati mwingine mahusiano yasiyokuwa salama na kusababisha kupata mimba ama magonjwa ya zinaa.

“Kwa hiyo elimu ya afya ya uzazi kwetu sisi ni muhimu sana kuwawezesha mabinti ili kuwatoa kwenye wimbi la kupata mimba zisizotarajiwa, wajitambue wanapokuwa, vitu gani wanaweza kuviona kwenye miili yao kwa jinsi gani ya kuepuka mihemko ambayo inasababisha kupata ujauzito usiotarajiwa,” amesema.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Macho kwa Jamii, Theresia Lihanjala amesema wamekutana na wanawake 10, kati yao mabinti sita na wanawake wanne katika mradi wa ‘Binti Songa Mbele’ unaolenga kuwasaidia kutoka kwenye changamoto za kiuchumi wanazokutana nazo.

“Lengo ni kukusanya mawazo ya pamoja wawe na wazo ambalo watachakata wapate mradi ambao tutaufadhili, ili tuende nao pamoja na kuwawezesha kiuchumi,” amesema.

Amesema wengi ya wanawake hao ni wale walioshindwa kuendelea na masomo, wengine walisoma lakini hawakufanikiwa kujiendeleza na wengine ni wamama wa nyumbani wanaolea familia.

Amesema lengo la kuwawezesha kiuchumi ni kuwakwamua wasiwe tegemezi kwa sababu wanapokuwa tegemezi ndio wanafanyiwa mambo ya ukatili au kujiingiza kwenye mahusiano yasiyotarajiwa, na baadaye kunakuwa na familia zisizotarajiwa.

“Na wamama pia kwa kuwa wamekuwa ni watetezi wa haki za watoto , hivyo wamama wengi wana nafasi kubwa ya kufanya malezi, sasa wanapokosa hali nzuri ya kiuchumi husababisha familia kutokuwa imara.

“Huu mradi utamsaidia huyu mama kuwa na kitu chake cha kufanya cha kuweza kuzalisha aidha akazalishe katika mazingira ya nyumbani au anaweza kuzalisha kwa umoja wao lakini atakuwa na uhakika, anamka asubuhi anafanya hiki na kinamuingizia kipato,” anasema.

Naye Cecilia Mtagwa amesema anatarajia kupata elimu itakayomwezesha kujua kushona mitindo ya aina mbalimbali za nguo ambayo ataitumia kuwafundisha wengine.


No comments:

Post a Comment

Pages