HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 07, 2024

DAWASA yaeleza mafanikio, changamoto miaka mitatu ya Rais Samia

NA MWANDISHI WETU

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), limeeleza mafanikio iliyoyapata katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, amezungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari jijini Dar es Salaam leo Agosti 7, katika utaratibu uliowekwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kuelezea mafanikio ya taasisi za Serikali.

Akizungumza na wahariri hao, Mhandisi Bwire alisema DAWASA ambayo imepitia hatua mbalimbali za maboresho yaliyolenga ufanisi wa kuhudumia wateja, alisema taasisi yake imepata mafanikio makubwa katika uzalishaji na uanzishwaji wa miradi mipya.


“Uwezo wa uzalishaji maji umeongezeka kutoka lita milioni 520 kwa siku mpaka lita milioni 534.6 kwa siku, ambalo ni sawa na ongezeko la lita milioni 14.6 kwa siku. Hii ni pamoja na ongezeko la uwezo wa DAWASA katika kuhifadhi maji.

“Uwezo wa kuifadhi maji umeongezeka kutoka lita milioni 153.64 hadi lita milioni 183.64 sawa na ongezeko la lita milioni 30, huku mtandao wa usafirishaji na usambazaji maji ukiwa umeongezeka kutoka kilomita 4,690.7 hadi kilomita 7,087,” alisema Bwire.

Aliongeza ya kuwa, mtandao wa majitaka nao umeongezeka kutoka kilomita 450 hadi kilomita 517.12, ambalo ni sawa na ongezeko la kilomita 67.12, huku idadi ya maunganisho ya wateja wa majisafi ikiongezeka kutoka 343,019 hadi 438,177.

“Kila palipo na mafanikio, changamoto hazikosekani, iko hivyo pia kwa DAWASA, ambayo inapambana na changamoto mbalimbali zikiwemo za mabadiliko ya tabia nchi, ujenzi wa bwawa la Kidunda, elimu kwa wananchi na uvamizi na uharibifu wa vyanzo vya maji.

“Changamoto zingine zinazoikabili DAWASA ni pamoja na ujenzi wa makazi usiozingatia taratibu za mipango miji, ushirikiano na wadau (Tanroads, Manispaa) kutatua changamoto na uvamizi katika maeneo ya hifadhi ya miundombinu ya maji,” alibainisha.

Kwa mujibu wa Mhandisi Bwire, uchakavu wa mabomba na upotevu wa maji ni miongoni mwa changamoto zinazokwaza uendeshaji wa taasisi hiyo, ikiwa ni pamoja na madeni ya wateja, kutenga fedha za ndani kila mwaka na kutafuta fedha za mikopo nafuu.

“DAWASA tunaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kulipia huduma, huku tukiwa na uhitaji mkubwa wa fedha kwa ajili ya uwekezaji ili kufikia malengo kwa wakati, pamoja na kushirikisha wizara ya fedha na wadau wengine kuona njia mbadala ya kugharamia miradi.

“Na miongoni mwa miradi mipya inayoendelea ni pamoja na Mradi wa Maji Dar es Salaam ya Kusini, ambao mkataba wake ulisainiwa Oktoba 31, 2023, ambao utakuwa ujenzi wa tenki la ujazo lita milioni 9, mradi ambao una thamani ya Sh. Bilioni 34.5,” alifafanua.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tazania (TEF), Deodatus Balile, aliipongeza DAWASA kwa mafanikio makubwa, aliyoyataja kuwa yanatokana na utendaji mzuri wa Kaimu Afisa Mtendaji huyo anayeamini kwamba ana sifa zote za kuendesha taasisi hiyo muhimu.

Aliitaka kupambana kumaliza changamoto zilizopo ili kuongeza ufanisi wa taasisi katika kuwahudumia wananchi, huku akimtaka kuepuka watendaji wasiopenda kuwajibika na kuwajibisha wazembe.

“Upotevu wa maji ni mkubwa, utakuta mitaani kumetapakaa maji na kuzalisha madimbwi makubwa, lakini hakuna hatua za makusudi zinachokuliwa kwa haraka kuzuia uharibifu huo. Upotevu wa maji hauepukiki katika usambazaji wa maji, lakini unaoshuhudiwa ni mkubwa sana.

“Tunatamani kuona DAWASA muende mbali zaidi mufunge mita za maji kila mtaa, kila kata, hii itasaidia kuona haya maji yanapotelea wapi. Na katika hili la ‘smart meter’, nashauri taasisi iangalie mita zinazotengenezwa na wazawa, hizi za kigeni hazina ubora,” alieleza Balile.



No comments:

Post a Comment

Pages