HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 15, 2024

RITA yatoa vyeti kwa watoto milioni 10


Naibu katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Khatibu Kazungu (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja  mara baada ya kukabidhi  vyeti vya  kuzaliwa  kwa wananchi wakati wa maadhimisho ya siku ya Usajili wa matukio muhimu ya Binadamu na takwimu Barani Afrika  yanayoadhimishwa   kila ifikapo  tarehe 10 Agosti kila  mwaka, yaliyoadhimishwa kitaifa Jijini Dodoma mwishoni  mwa  juma lililopita. Wa tatu kushoto ni Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) Bw. Frank Kanyusi na watatu kulia ni Afisa Hifadhi wa Watoto kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Asnath Barnabas.

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imeipongeza Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa kazi nzuri wanayoifanya ikiwemo utoaji utoaji bure wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto  chini ya umri wa miaka mitano Tanzania bara.

Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya  watoto milioni 10,  ambao ni sawa na asilimia 68 wameshasajiliwa  katika mikoa yote 26 Tanzania bara  nakupewa vyeti vya kuzaliwa, ukilinganisha na asilimia 13 wakati wanaanzisha mpango huo mwaka 2012.

Akizungumza   wakati wa maadhimisho ya siku ya Usajili wa matukio muhimu ya binadamu na takwimu Barani Afrika, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Dk Khatibu Kazungu amesema hatua hiyo ni ya kupongezwa.

Amesema kuwa serikali  kupitia RITA imeanza kuchukua hatua madhubuti  ya kuongeza kasi ya usajili kupitia mkakati wa kitaifa wa usajili wa matukio muhimu ya binadamu  na  takwimu.

“Kila ifikapo Agosti 10 kila mwaka, Tanzania inaungana na mataifa mengine Barani Afrika kuadhimisha siku hii muhimu iliyobeba kauli mbiu isemayo ‘ Kuimarisha  Uhusiano wa Usajili  wa Matukio Muhimu ya  Binadamu na Takwimu na Mifumo  ya Kisheria ya  Utambuzi kwa njia ya Kidijitali iliyo jumuishi,” ameeleza, Dkt. Kazungu.

Aidha Dk Kazungu amesema serikali kwa kushirikiana  na wadau wa maendeleo  wataendelea kuweka  mikakati ya kuhakikisha  mpango  wa kuwasajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto wa umri chini ya miaka 5 unakuwa endelevu  kwa kuhakikisha kila mtoto  anayezaliwa anapata fursa ya kusajiliwa ndani ya muda mfupi na taarifa zao zinatumwa kwenda kwenye kanzidata ya RITA  kwa  wakati stahiki.

“Nitoe rai kwa wazazi kuhakikisha wanatumia fursa hii iliyotolewa na serikali ili kuwapatia watoto wao vyeti vya kuzaliwa ambavyo ni nyaraka ya msingi ya utambulisho.” amesisitiza, Dk Kazungu

 Dk Kazungu amesema Usajili wa matukio yote muhimu ikiwemo vizazi, na vifo unaiwezesha serikali kupata takwimu sahihi kwa ajili ya kupanga mipango endelevu ya maendeleo  kwa maslahi  mapana ya taifa.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA Frank Kanyusi amesema maadhimisho hayo ya Nane Nane ambayo kitaifa  huadhimishwa jijini Dodoma, yamelenga kujenga ufahamu kwa wananchi juu ya kumbukumbu muhimu pamoja na matukio muhimu ya vizazi, vifo, talaka, ndoa pamoja na kuasili watoto.

“Katika kuadhimisha  siku hii, kuna shughuli mbalimbali ambazo  tunazifanya, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu  kwa umma, kutoa huduma za usajili sambamba  na kutembelea  vituo vinavyofanya usajili  wa matukio muhimu ya binadamu ili kubaini changamoto na kuzitafutia  ufumbuzi,” amesem Kanyusi.

Kwa upande wake, Afisa Hifadhi wa Watoto kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF),  Asnath Barnabas, mbali ya kuipongeza serikali kwa jitihada inazochukua katika kuhakikisha  wanawafikia  watoto wote  chini ya umri wa miaka mitano katika mikoa yote Tanzania bara na kutoa vyeti bure , alisema UNICEF wataendelea  kushirikiana na serikali ili kuhakikisha wanafikia malengo waliyojiwekea.

“Tutaendelea  kushirikiana na Serikali ya Tanzania na wadau mbalimbali wa maendeleo  katika kuhakikisha watoto wote wanasajiliwa na kupewa vyeti sambamba na  kuchukua kumbukumbu ya matukio yote muhimu ikiwemo vizazi, na vifo,” amesema Barnabas.

No comments:

Post a Comment

Pages