Na Mwandishi Wetu, Dodoma
BALOZI wa Marekani nchini Tanzania Michael Battle, amewataka wakulima nchini kuchangamkia fursa ya mazao ya parachichi, kahawa na korosho ambayo yana soko la uhakika kwao.
Baadhi ya mabanda aliyoyatembelea Balozi Battle ni la wadau wa Kilimo Ikolojia Hai chini ya Island of Peace (IDP), Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Taasisi ya Wakulima wa Mbogamboga na Matunda Tanzania (TAHA) na wengine.
Balozi Battle amesema Wamarekani wanatumia parachichi, kahawa na korosho kwa wingi kutoka nchi za Marekani ya Kusini ikiwemo Mexico hivyo amewataka wakulima wa Tanzania kuchangamkia fursa hiyo ambayo soko lake lipo wazi.
“Sisi Marekani kupitia USAID tumekuwa tukifadhili wakulima katika nyanja mbalimbali na kusema ukweli tunajisikia faraja kwani kuna matokeo chanya, ila napenda kutumia nafasi hii, kuwahamasisha wakulima nchini Tanzania kulima kwa wingi mazao ya parachichi, korosho na kahawa ambayo yanahitajika kule kwetu,” amesema.
Balozi Battle amesema ili mazao ya Tanzania yaweze kupata soko la uhakika Marekani ni lazima wakulima kuzingatia kilimo ikolojia hai.
Amesema kilimo ni moja ya eneo likiwekewa mkazo linaweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kiafya.
Balozi amesema wanaridhishwa na ufanisi wa miradi ambayo wanayofadhili hasa kilimo, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora, ili kuwa na uhakika wa soko.
Battle amesema Marekani itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kilimo na mingine nchini Tanzania.
Akizungumzia msaada wa USAID katika kilimo, Mkurugenzi Mkazi wa Island of Peace (IDP), Ayesiga Buberwa amesema Marekani wameweza kugusa wakulima katika eneo la kutunza, kuhifadhi na kuendeleza mbegu asili.
Buberwa amesema USAID imewezesha vijana kujikita katika kilimo, hasa katika eneo la kuongeza thamani kwenye mazao na kutengeneza mbolea asili kwa kutumia mbinu mbalimbali.
“Sisi Island of Peace tunawashukuru watu wa Marekani kwa kufadhili wakulima wadogo ambao sasa wanaanza kupata manufaa, kimsingi tunaendelea kuwaomba USAID kusaidia zaidi,” amesema.
Mkurugenzi huyo lengo lao ni kupanua wigo hasa kwa kufikia wakulima wadogo ambao wapo vijijini, kwa sababu zina manuufaa kwenye kuhifadhi mazingira, ardhi na kustawi kwa kipato cha mkulima.
“Tunafanya kazi na wakulima wadogo kabisa takribani 3,500 lakini pia tupo na Shirikisho la Vyama vya Wakulima na Wafugaji Tanzania (SHIWAKUTA), ambalo lina wanachama zaidi 45,000, ni imani yetu kwa ushirikiano huu tutaleta mapinduzi kwenye kilimo,” amesema.
Buberwa amesema wanafanya kazi zaidi katika mkoa wa Arusha, ila kupitia SHIWAKUTA watafika mbali zaidi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT, Geofrey Kirenga amesema kwa kushirikiana na USAID wameweza kufikia takribani wakulima 400,000 ambao wanajihusisha na kilimo cha mazao 12.
Kirenga amesema USAID imekuwa ikichochea ukuaji wa kilimo kwa asilimia kubwa katika ukanda wa SAGCOT na matokeo yamekuwa mazuri, hali ambayo inasababisha waanze kufikiria kwenda nchini kote.
“Tunafurahi kuona Marekani kuwa sehemu ya kukua kilimo ukanda wa SAGCOT na tumeweza kufikia wakulima takribani 400,000 ambapo mazao 12 yanahusika kwenye mradi,” amesema.
Ametaja baadhi ya mazao hayo ni nyanya, chai, viazi, soya, nafaka, mbogamboga na mengine, hali ambayo inaifanya mikoa ya Kusini kutambulika kama kapu la chakula.
Aidha, Kirenga amesema pia SAGCOT kwa kushirikiana na USAID imesaidia ujenzi wa miundombinu kama barabara ambayo inayoelekea wilayani Kilombero na kwingineko.
Kirenga amesema USAID imechochea mahusiano mazuri kati ya Tanzania na Marekani, huku akiweza bayana kuwa mauzo yameongezeka nchini humo.
“Kuna ongezeko la biashara kati ya Marekani na Tanzania na Balozi Battle amesema kuna soko la chokileti, korosho, mafuta ya parachichi na mengine, naomba tuchangamkie fursa hii,” amesema.
No comments:
Post a Comment