HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 09, 2024

BALOZI NCHIMBI AWEKA NENO UPATIKANAJI WA NIDA NGARA

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel  Nchimbi ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa Vitambulisho vya Uraia (NIDA) kwa wananchi wa Ngara, mkoani Kagera, wanaokidhi vigezo.

Nchimbi ameyasema hayo Agosti 7, 2024 alipokuwa akizungumza na maelfu ya wananchi wa Mji wa Ngara, katika Uwanja wa Posta, akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Kagera, baada ya Mbunge wa Jimbo la Ngara Mhe. Ndaisaba Ruhoro kuwasilisha kilio hicho kwenye mkutano huo.

Mapema pia kabla ya mkutano wa hadhara huo, Balozi Nchimbi alitoa maelekezo kuhusu suala hilo la upatikanaji wa vitambulisho vya NIDA, aliposimama kuwasalimia  wananchi wa Kijiji cha Kumunazi  alipokuwa njiani akitokea Biharamulo, kueleeka Ngara.

Akiwa ameambatana na wajumbe wa Sekretarieti ya CCM Taifa katika ziara hiyo; Ndugu Issa Haji Usi Gavu, Ndugu Amos Makalla na Ndugu Rabia Abdallah, Balozi Nchimbi ameielekeza Wizara hiyo kuchukua hatua haraka ili changamoto hiyo imalizwe.

Amesema hata utaratibu wa kuruhusu watu kuazimana vitambulisho vya NIDA kwa shughuli mbalimbali ni jambo hatari, linaloweza kusababisha uhalifu.

"CCM itasimamia ili kuhakikisha suala hilo linafanyiwa kazi na kasi ya utoaji wa vitambulisho vya NIDA inapatikana," amesema Dk. Nchimbi.


 

No comments:

Post a Comment

Pages