Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Peter Msoffe amewaomba wadau wa maendeleo kuendelea kuchangia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia nchini Tanzania ili kuwawezesha wananchi kuacha kukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa hivyo kulinda afya na mazingira.
Ametoa wito huo wakati akishiriki uzinduzi wa
mpango wa nishati safi ya kupikia shuleni ambao unalenga kuziwezesha taasisi
hizo za elimu kutumia nishati safi ya kupikia, uliofanyika pembezoni mwa
Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea
katika Jiji la Belem nchini Brazil.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa nishati safi ya
kupikia ameonesha dhamira ya dhati ya kuwezesha upatikanaji wa nishati hiyo.
Ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia amekuwa
akichagiza ‘Agenda 300’ ambayo inalenga kupeleka umeme kwa Waafrika milioni 300
ifikapo mwaka 2030 hivyo itasaidia wananchi kutumia umeme wa gharama nafuu na
kuacha kutumia nishati isiyo rafiki kwa mazingira.
Prof. Msoffe amesema kuwa dhamira ya Serikali
ni kuhakikisha nishati hiyo inapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu ili
kumuwezesha kila Mtanzania kumudu.
Amesema kuwa pamoja na Serikali kutoa
maelekezo kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kuachana na kuni na mkaa,
inaendelea kuchagiza elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi
ya kupikia.
Pia, ameeleza kuwa bado wananchi wanahitaji
kupata nishati safi ya kupikia ambapo inatarajiwa kuwa ifikapo mwaka 2034
asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi na kuachana na kuni na
mkaa kwa ajili ya kupikia.
Aidha, Prof. Msoffe amewashukuru wadau wa
maendeleo wakiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP) kwa
kuanzisha program hii kwenye shule na kuwahakikishia Tanzania itaendelea kuwapa
ushirikiano ili kuleta maendeleo endelevu.
Amesema mpango huo si tu unaziwezesha shule
kupata nishati safi ya kupikia bali pia unawajenga wanafunzi kuwa mabalozi wa
matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa jamii inayowazunguka.
Kwa upande wake Mshauri wa Masuala ya Nishati
kutoka WFP Tanzania Bw. Geofrey Ndegwa WFP amesema shule ni sehemu muhimu ya
kuwekeza agenda ya nishati safi ya kupikia kwani wanafunzi wanapata ufahamu
kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati hiyo.
Amepongeza juhudi za Serikali za kuhakikisha
taasisi zote za elimu zinaanza kutumia nishati safi ya kupikia kwakuwa
zinahudumia idadi kubwa ya watu (Zaidi ya 100) hivyo kutumia kuni na mkaa kwa
wingi na kusababisha miti kukatwa kwa wingi.
Bw. Ndegwa ametoa wito kwa Serikali
kushirikiana na wadau wakiwemo Shirika la WFP katika kuchagiza agenda ya
nishati safi ya kupikia katika shule zote hatua itakayosaida kukabili athari za
mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na ukataji wa miti.
Nae Profesa Ed Brown kutoka Program ya Moden
Energy Cooking Service amesema kuna fursa kubwa katika kuziwezesha nchi za
Afrika ikiwemo Tanzania kupata nishati safi ya kupikia.
Amesema ni wakati sasa sekta binafsi zikashirikiana na Serikali katika kuhakikisha agenda ya nishati safi ya kupikia inakua na kusambaa kwa jamii.






No comments:
Post a Comment