HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 18, 2025

DKT. MWIGULU: AMANI HAICHEZEWI, WATANZANIA WOTE TUILINDE

*Asisitiza wananchi kujiepusha na watu wenye nia ovu na Taifa lao

 

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania wote kuendelea kuwa makini na kujiepusha na watu wenye nia ovu dhidi ya Tanzania ambao wamekuwa wakihamasisha vurugu ili kuvuruga amani na kuathiri shughuli za kiuchumi na kijamii.

Waziri Mkuu Mwigulu ametoa rai hiyo leo Desemba 18, 2025 alipozungumza na wakazi wa Kiwira mkoani Mbeya akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu ya umma na mali za watu binafsi ambazo zimeathirika na vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025.

“Tunaelewa lengo lao ni rasilimali zetu, Tanzania ina rasilimali adhimu barani Afrika na wanajua ili kuzipata ni lazima kuwavuruga Watanzania, hili jambo msikubali, amani yetu ndio kila kitu. Tunapaswa kuendelea kushirikiana kulinda amani.”

Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ameendelea kusisitiza kwamba pahali ambapo hapana amani hakuna shughuli yoyote ya maeneleo ambayo inaweza kufanyika, hivyo amewahimiza wananchi hususan vijana kuwa makini na kutokubali kutumika.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesisitiza watumishi wa umma kuendelea kuwahudumia wananchi ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuwafuata katika maeneo yao, hususani ya pembezoni ili kuwasikiliza na kushirikiana nao kutatua changamoto zao.

Pia, Waziri Mkuu amewataka watendaji wa sekta ya afya kuhakikisha vituo vya kutolea huduma za afya nchini zinakuwa na dawa za kutosha na wanapoagiza dawa wahakikishe wanafanya tafiti na kuagiza dawa kutokana na mahitaji ya eneo husika.

Kabla ya kuzungumza na wananchi Waziri Mkuu alikagua majengo ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kyela na majengo ya Ofisi ya Kituo cha Forodha kwa Pamoja-Kasumulu ambayo ni miongoni mwa ofisi za umma zilizoathiriwa na vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025.

No comments:

Post a Comment

Pages